Mrembo wa kuonyesha mavazi Naomi Campbell atoa ushahidi dhidi ya Dikteta Charles Taylor | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mrembo wa kuonyesha mavazi Naomi Campbell atoa ushahidi dhidi ya Dikteta Charles Taylor

Kwa muda wa miaka 11, hadi mwaka 2002 vilizuka nchini Sierra Leone vita vya wenyewe kwa wenyewe, sababu ya vita hivyo kuchukua muda mrefu ni biashara haramu ya madini ya almasi.

Mrembo wa kuonyesha mavazi raia wa Uingereza Naomi Campbell ametoa ushahidi hii leo katika kesi inayomuhusisha dikteta wa zamani wa Liberia Charles Taylor kuhusu zawadi aliyopewa ya almasi katika mahakama ya kimataifa mjini The Hague.

Mrembo wa kuonyesha mavazi raia wa Uingereza Naomi Campbell ametoa ushahidi hii leo katika kesi inayomuhusisha dikteta wa zamani wa Liberia Charles Taylor kuhusu zawadi aliyopewa ya almasi katika mahakama ya kimataifa mjini The Hague.

Kwa muda wa miaka 11 , hadi mwaka 2002, vilizuka nchini Sierra Leone vita vya wenyewe kwa wenyewe . Sababu iliyofanya vita hivyo kuchukua muda mrefu kiasi hicho , ni biashara ya almasi ambayo ilikuwa ikitumiwa kugharamia makundi ya waasi. Charles Taylor alikuwa wakati huo rais wa nchi jirani ya Liberia. Ameshiriki katika biashara hii ya almasi na kusaidia kuendeleza vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. Anashtakiwa kwa hiyo kwa mauaji, kuwaandikisha watoto jeshini, kusababisha ulemavu, na uporaji , katika mahakama maalum kuhusu Sierra Leone katika mji wa The Hague nchini Uholanzi.Taylor amekana mashtaka hayo . Mahakama hiyo imekuwa na wasi wasi hata hivyo kutokana na shahidi wake huyo anayefahamika sana.

Siku moja katika mwaka 1997, mrembo huyo wa kuonyesha mavazi ambaye ni maarufu duniani Naomi Campbell alihudhuria hafla iliyoandaliwa na rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela. Katika hafla hiyo alikutana pia na kiongozi huyo wa zamani wa Liberia Charles Taylor. Taylor alivutiwa sana na uzuri wa Naomi ambapo baada ya hafla hiyo alimzawadia almasi ambazo hazijakatwa katika chumba chake cha hoteli alimofikia. Leo hata hivyo anaonna na mtu huyo aliyemhusudu lakini mara hii akiwa kizimbani katika mahakama hiyo na anatakiwa kutoa ushahidi dhidi yake.

Kesi hiyo ambayo ilianza kwa mara ya kwanza Januari 2008, ni ya kwanza kwa rais aliyekuwa akitawala barani Afrika ameweza kufikishwa mahakamani. Ni kesi inayofungua njia, kama Elly Harrowell kutoka katika shirika la kutetea haki za binadamu nchini Uingereza , Global Witness anavyoelezea.

Aina hii ya kesi inatoa ishara ya wazi, kuwa yule ambaye atafanya uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu , atafikishwa katika mkono wa sheria. Na Charles Taylor atawajibishwa kwa kile alichokifanya.

Mrembo huyo wa kuonyesha mavazi Naomi Campbell amewaambia waendesha mashtaka katika mahakama ya kimataifa kuwa alipewa almasi hizo kama zawadi nchini Afrika kusini mwaka 1997, lakini hakufahamu iwapo madini hayo ambayo yalikuwa machafu yalitolewa na rais wa zamani wa Liberia dikteta Charles Taylor.

Amesema kuwa almasi hizo alipewa zikiwa katika kisanduku cha vito katika hoteli alimofikizia na watu wawili, lakini akaongeza kuwa hakuuliza kisanduku hicho kinatoka kwa nani.

Alifungua kisanduku hicho siku ya pili, anasema. Aliona mawe machache. Yalikuwa madogo na yalionekana machafu.

Mrembo huyo amesema kuwa aliambiwa wakati wa kifungua kinywa asubuhi na mcheza sinema kutoka Marekani Mia Farrow pamoja na mshauri wake wa masuala ya mahusiano kuwa mawe hayo huenda ni ni almasi ambazo hazijakatwa ambazo huenda zimetumwa na Charles Taylor.

Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo Brenda Hollis amesema kuwa anamatumaini ya kuthibitisha kutokana na kauli ya Campbell kuwa dikteta huyo wa zamani wa Liberia alikuwa na kile kinachoitwa almasi za damu, zilizopatikana kutoka katika maeneo ya waasi ili kugharamia ununuzi wa silaha za mamilioni ya dola kwa ajili ya Sierra Leone.

Mwandishi : Shale, Andrew / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman

E N D E

 • Tarehe 05.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OcTM
 • Tarehe 05.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OcTM
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com