1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi wa kijamii Neukölln

Ripperger, Sabine13 Agosti 2008

Jinsi mradi mdogo wa kuwajumuisha wageni katika maisha ya kila siku ya kijamii huko Berlin-Neukölln,unavuvutia miji na nchi jirani

https://p.dw.com/p/EwHs
Mkahawa wa "Al Salam "huko Neukölln mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa


Mradi mdogo wa mtaa wenye wakaazi wengi wenye asili ya kigeni, Berlin-Neukölln,umegeuka kua jumuia ya aina pekee ya kijamii.Mradi huo uliopewa jina "Mama wa Mtaa" unawaleta pamoja wakinamama vijana,wengi wao ni wenye asili ya kituruki na kiarabu na wenye watoto pia,wakipatiwa mafunzo ya miezi sita katika fani ya elimu na afya."Shughuli za "mama wa mtaa"ni pamoja na kuzitembelea familia na kuzungumza nazo kwa lengo la kurahisha juhudi za kuzijumuisha familia hizo katika maisha ya kila siku ya kijamii.Mradi huo unagharimiwa kwa pamoja na serikali ya mtaa wa Neukölln,baraza la utawala la jiji la Berlin na kituo cha kuwatafutia watu kazi.Mama wa Mtaa wana ofisi yao pia katika baraza la jiji la Neukölln.


Tangua mwaka 2000,waasisi wa mradi huo,wakiwemo wazee na wasimamizi wa shule za chekechea,wakuu wa shule pamoja pia na wawakilishi wa mashirika yanayopigania masilahi ya wahamiaji na mashirika ya ushauri,walianza kutafakari matatizo yanayozikumba familia katika eneo lao.Kwa manenao mengine matatizo ya ukosefu ajira na viwango vya chini vya elimu katika eneo hilo lenye wakaazi wengi wenye asili ya kigeni.Zaidi ya thuluthi moja ya wakaazi wa eneo hilo la Neukölln,kijerumani sio lugha yao ya mama na zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa kwenda katika shule za chekechea,hawapelekwi katika vituo hivyo.Mara nyingi wazee wanajikuta wakizidiwa,wanashindwa kutekeleza majukumu yao linapohusika suala la ulezi na elimu ya watoto.Ili kukomesha hali hiyo,ukaanzishwa mradi wa "Mama wa Mtaa" mnamo mwaka 2004,mradi unaowavutia hivi sasa wakaazi wa maeneo mengine pia ya jiji la Berlin na kwengineko kote nchini Ujerumani.


Awali mradi huo ulituwama katika eneo moja tuu la mtaa wa Neukölln.Hivi sasa,anasema mkuu wa mradi huo Maria Macher,mradi huo umekua mkubwa..Lakini nini kinachoufanya mradi huo uwe wa aina Pekee?Bibi Maria Macher anatueleza:


"Kusema kweli kitu cha aina pekee kabisa katika mradi wetu ni ile hali kwamba tunawapatia mafunzo wakinamama ambao hawana asili ya kijerumani,wengi wao wana asili ya kiarabu na kituruki,na ambao baada ya kuhitimu mafunzo  wanakua wakiwapatia maelezo mama wengine kama wao kuhusu fani za ulezi,elimu na afya.Wakinamama wanaketi na wanawake wenzao na kuzungumza  lugha moja,lugha yao ya mama.Tunatumia pia vijarida vilivyoandikwa kwa lugha hizo hizo.Na kwa kua wakinamama hao wanazijua tamaduni,lugha, na hata desturi za familia hizo,wanakua na kazi rahisi wakilinganishwa kwa mfano na mtaalam wa masuala ya kijamii wa kijerumani."


Wanaosaidiwa katika mpango huo sio tuu familia,bali pia wakinamama ambao kwa muda mrefu wamekua hawana ajira.Kutokana na mradi huo,kila mwanamke mmoja hupatiwa pato japo dogo- yuro 180 kwa kuzitembelea familia kumi pamoja pia na kupatiwa mafunzo ya kazi.Wakati huo huo Mama wa Mtaa wanajitolea katika shughuli zao nyengine bila ya malipo,mfano wanatoa ushauri kwa njia ya simu na kadhalika.


Mradi huo umekua hivi sasa.Wakinamama 140 wanachangia kuzitembelea familia nyengine kila siku.


Mradi huo umeenea pia katika mitaa mengine ya Berlin,Kreuzberg na Steglitz,kwengine nchini Ujerumani na hata nje ya nchi hii.


Nchi jirani ya Danemark nayo pia inavutiwa na mradi huo na kuuanzisha katika mitaa yake sabaa.