1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Mpwa wa Khamenei autaka ulimwengu kukata uhusiano na Iran

29 Novemba 2022

Farideh Moradkhani, mpwa wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ametoa wito kwa watu kuzishinikiza serikali zao kusitisha uhusiano na Tehran juu ya ukandamizaji wake kwa maandamano dhidi ya serikali hiyo.

https://p.dw.com/p/4KDAN
Iran | Farideh Moradkhani
Picha: Harana

Katika video iliyowekwa mtandaoni na kaka yake anayeishi Ufaransa, Farideh Moradkhani, aliwataka "watu wenye ufahamu ulimwenguni'' kuwaunga mkono waandamanaji wa Iran. Video hiyo ilirushwa mtandaoni wiki hii baada ya kuripotiwa kukamatwa kwa Moradkhani Novemba 23, kulingana na shirika la Marekani la uatiliaji wa haki (HRANA).

Iran | Präsident Ebrahim Raisi
Rais wa Iran, Ebrahim RaisiPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Moradkhani ni mwanaharakati wa muda mrefu ambaye marehemu baba yake alikuwa mpinzani maarufu na alimuoa dada yake Khamenei na ndiye mwanafamilia wa karibu zaidi wa kiongozi mkuu huyo kukamatwa. Upande huo wa familia umekuwa ukimpinga Khamenei kwa miongo kadhaa na Moradkhani amekuwa akifungwa jela mara kadhaa kutokana na harakati zake.

  Soma zaidi: Iran yalaani uchunguzi wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa

Katika taarifa yake ya video Farideh alisema: " Nawaomba watu makini wa dunia kusimama nasi na wazishinikize serikali zao wasijibu kwa kauli mbiu na maneno matupu bali kwa kuchukua hatua za kweli na kukomesha mahusiano yoyote na utawala huu."

Iran Kundgebung
Waandamanaji wa Iran wakidai haki za wanawake na kupinga kifo cha Mahsa AminiPicha: Farid Ashrafian/DW

Maandamano hayo, ambayo sasa yametimiza miezi mitatu, yamegubikwa na hali ya kikatili na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama vya Iran kwa kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuyazima maandamano hayo.

Maandamano yenye maafa makubwa

Ayatollah Ali Khamenei
Ayatollah Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa IranPicha: IRANIAN LEADER PRESS OFFICE/AA/picture alliance

Kulingana na shirika la wafuatiliaji wa haki HRANA, angalau watu 451 wameuawa, wakiwemo watoto 63, huku watu 18,173 wakizuiliwa. Licha ya ukandamizaji huo, maandamano yanaendelea na kusambaa katika miji mbalimbali.

Machafuko hayo yalichochewa na kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22

aliyefariki akiwa kizuizini mwa polisi wa maadili mjini Tehran kwa kukiuka sheria kali za mavazi kwa wanawake za Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Iran

Iran Sprecher Nasser Kanaani zur Messerattacke auf Salman Rushdie
Nasser Kanaani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje wa IranPicha: Iranian Foreign Ministry/AP Photo/picture alliance

Maandamano hayo yamegeuka na kuwa changamoto kubwa zaidi tangu Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979. Iran imesema pia kuwa haitashirikiana na ujumbe wowote wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ili kufichua ukweli kuhusu ukandamizaji mbaya wa maandamano hayo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Nasser Kanaani amesema siku ya Jumatatu kuwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kuanzisha misheni hiyo wiki iliyopita, lakini Jamhuri hiyo ya Kiislamu haitajihusisha na ushirikiano wowote na kamati waliyoiita ya kisiasa na inayojinadi "kutafuta ukweli".