1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpatanishi wa Iran aonya magharibi dhidi ya vitisho.

2 Aprili 2010

Mpatanishi wa Iran, Saeed Jalili alikutana wa washiriki wa China.

https://p.dw.com/p/MmIc
Mpatanishi wa Iran kuhusu mzozo wa nyuklia, Saeed JaliliPicha: AP

Kufikia sasa China imekataa kuunga mkono azimio la vikwazo vipya la nchi za magharibi dhidi ya Iran. Mapema leo China inataka nchi husika ziwe na mazungumzo zaidi na zisiwe na misimamo mikali ili kujaribu kutatua mzozo wa kimataifa unaohusisha Iran na nguvu za nyuklia.

Katika mazungumzo kwa njia ya simu na rais Hu Jintao wa China, rais wa Marekani Barack Obama ametoa mwito wa ushirikiano zaidi kuhakikisha kwamba Iran inazingatia matarajio ya kimataifa.

Mpatanishi mkuu wa Iran, Saeed Jalili hata hivyo alipendekeza kwamba China imeitikia mwito wa msaada unaohitajika na Iran.

Jalili aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo na washiriki wa China kwamba mambo mengo yalijitokeza katika mazungumzo yao na China ilikubali msimamo wa Iran. Jalili alikiri kwamba katika mazungumzo yaliyomhusisha waziri wa mambo ya nje wa China, Yang Jiechi kwamba suala la kuiwekea Iran vikwazo limekosa uzito.

Wizara ya mambo ya nje ya China bado haijatoa msimamo wake.

Mpatanishi Saeed Jalili alisisitiza kwamba nchi za magharibi zinafaa kubadilisha mbinu zao zisizofaa na ziache kuitishia Iran. Alionya kwamba mazungumzo na nchi sita zenye ushawishi mkubwa ikiwemo China na Marekani yanaweza kusambaratika ikiwa nchi za magharibi hazitasisisha vitisho vyake.

Jalili alisema kwamba ikiwa vitisho vitashamiri basi mazungumzo hayawezi kufaulu. Aliongeza kwamba China kama nchi kubwa inaweza kujihusisha kubadilisha mbinu zisizofaa katika kukabiliana na Iran.

Nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwemo Uingereza, Ufaransa, Urusi, Marekani na Ujerumani zimekuwa zikihusika kwa mazungumzo na Iran kwa miezi kadhaa kujaribu kutanzua mzozo wa nyuklia wa Iran.

Barack Obama (L) and China's Präsident Hu Jintao Flash-Galerie
Rais Obama wa Marekani na Hu Jintao wa China. Marekani inaiomba China iipe mbinyo Iran kuhusu suala la nyuklia.Picha: Landov

China ina uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na kibiashara na Iran inayohusisha ununuzi wa mafuta na mali ghafi za nishati.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice alisema China iko tayari kwa mazungumzo ya ziada, hatua iliyopigiwa upatu na Ikulu ya Marekani kama mkakati unaofaa.

Urusi pia imesalia kimya kuhusu suala la kuiwekea Iran vikwazo vipya. Marekani na washirika wake wanashuku kwamba Iran ina njama ya kuunda silaha za kinyuklia ingawa Iran imesisitiza kwamba matumizi yake ya nyuklia sio ya madhumuni ya kuunda silaha na kwamba ina haki ya kuimarisha teknolojia ya nyuklia.

Mwandishi, Peter Moss/Reuters/AFP

Mhariri, Othman Miraji