1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa REDD wa Umoja wa Mataifa kujadiliwa Cancun

7 Desemba 2010

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa Cancun Mexico wajadili mpango wa kuzuia utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kwa ajili ya kuilinda misitu kwa kifupi, REDD

https://p.dw.com/p/QRLr
Waandamanaji wakipinga mpango wa REDDPicha: AP

Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo shirika la mazingira, UNEP, shirika la maendeleo, UNDP na shirika la chakula na kilimo, FAO, yameungana kuanzisha mpango wa kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kutokana na ukataji na uharibifu wa misitu, unaojulikana kwa kifupi kama REDD.

Mpango huo ulioanzishwa mnamo mwaka 2008 ni mfuko wa kimataifa unaowapa fursa wafadhili kuchanga fedha kwa lengo la kupunguza utoaji wa gesi chafu kutokana na uharibifu wa misitu katika nchi zinazoendelea. Kupitia miradi yake tisa ya kwanza barani Afrika, Asia na Amerika Kusini, mpango wa REDD wa Umoja wa Mataifa unasaidia uwezo wa serikali kutayarisha na kutekeleza mikakati ya kupunguza uharibifu wa misitu na utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kwa kuwajumuisha washikadau wote.

Mratibu wa mpango wa REDD wa shirika la mazingira la Greenpeace, Christoph Thies, amesema, "Mpango wa REDD unahusu misitu ya nchi zinazoendelea, ambazo zinahitaji kusaidiwa kifedha, ili ziweze kuilinda vyema zaidi misitu yao kutokana na majanga ya moto na uharibifu, kwa sababu uharibifu huu wa misitu husababisha athari kubwa za utoaji wa gesi zinazochagua mazingira. Ili kuzuia athari hizo, kunahitajika fedha kutoka kwa nchi zilizoendelea kiviwanda."

Mkataba wa haki wa mabadiliko ya tabia nchi ungekuwa ule unaoziwajibisha nchi zilizoendelea kiviwanda kutokana na jukumu lao kihistoria katika kusababisha utoaji wa gesi chafu ya carbon, na mabadiliko ya tabia nchi. Na kwa kuwa hekta moja la shamba la minazi au shamba la kilimo huleta fedha nyingi zaidi kuliko hekta ya msitu, sharti fedha zilipwe wale wanoilinda misitu, ili iendelee kuwepo. Hilo ndilo wazo linalozingatiwa na mpango wa REDD.

Swali litakalojitokeza kwenye mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi ni: Nani anayemiliki misitu? Na ni nani anayepaswa kupokea fedha kutoka kwa mpango wa REDD? Lars Lövold, mkurugenzi wa Mfuko wa kulinda misitu nchini Norway, anasema, "Nafikiri mkataba wa tabia nchi na misitu wenye haki, unahitaji kutambua haki za wakaazi asili wa misitu. Unahitaji kutayarishwa kwa uwazi na uaminifu kutoka ngazi za mashinani kwenda juu. Na njia pekee ya kuhakikisha fedha zinawafikia wale wanaoilinda misitu, badala ya kupotea kupitia rushwa, ni kuzingatia kanuni ya uwazi."

Bwana Lars aidha amesema kanuni hii ni msimamo wa kimaadili na suala la kimkakati. Amesema watu ambao wamekuwa wakiishi katika misitu wamekuwa na jukumu la kuilinda misitu ionekane mizuri kuliko kama hakungekuwa na watu wanaoishi ndani ya misitu hiyo. Amedokeza kuwa mpango wa REDD unajihusisha na juhudi kutafuta njia za kuwalipa fedha wale wanaoilinda misitu na kuwaadhibu wale wanaoiharibu.

Mwandishi: Jeppessen, Helle/ DW Cancun/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman