1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Konjunkturpaket Deutschland

Oumilkher Hamidou13 Januari 2009

Serikali kuu ya mjini Berlin yasifiwa kwa mpango wa kijasiri wa kupalilia shughuli za kiuchumi

https://p.dw.com/p/GXgO
Kansela Angela MerkelPicha: AP



Serikali kuu ya muungano mjini Berlin imeidhinisha mpango mkubwa kabisa wa kuinua uchumi,kuwahi kushuhudiwa katika historia ya baada ya vita nchini Ujerumani.Wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU na wale wa SPD wamekubaliana juu ya mpango wenye thamani ya takriban yuro bilioni 50.Mpango huo umetuwama zaidi katika kupunguza kodi ya mapato na matumizi mengineyo,pamoja pia na kuwekeza vitega uchumi katika mniradi ya miundo mbinu.Mashirika yatakayohitaji fedha taslimu,yatapatiwa mikopo itakayodhaminiwa na serikali.


Serikali kuu ya Ujerumani ilipoamua kwa mara ya kwanza kuinua shughuli za kiuchumi,mwaka jana,mpango uliokubaliwa ulikua dhaifu.Na hata wenyewe wameungama.Hivi sasa wakuu wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano wamepania kuhakikisha kila kitu kinapita barabara;wamepania kutoa kitita cha yuro bilioni 50 katika kipindi cha miaka miwili ijayo,ili kuzuwia shughuli za kiuchumi zisidorore na kuupa msukumo wakati huo huo ukuaji wa kiuchumi.


Ikiwa mtu atataka kuupatia noti mpango huo,kama inavyofanyika wanafunzi wanavyofanya mitihani shuleni,basi noti hiyo itakua kati ya "nzuri na mbaya".Pekee mpango wa uwekezaji ulioanuliwa na serikali kuu ya muungano ,ambao sehemu kubwa inatuwama katika miradi ya elimu,utagharimu yuro bilioni 18.Ni uamuzi wa kijasiri,na wa maana ambao unastahiki kupewa noti nzuri.Kwasababu serikali za majimbo na zile za miji zitaondokewa na mzigo mkubwa wa vitega uchumi, na kutia njiani miradi yake yote iliyokua hadi sasa imerundikizana makabatini.Inamaanisha kwa hivyo kupalilia pia ukuaji wa kiuchumi.


Serikali wakati huo itasamehe yuro bilioni tisaa zinazokusanywa kutoka kwa walipa kodi.Kwa hivyo wananchi watapunguziwa mzigo wa kodi na kwa namna hiyo kujipatia kiu cha kutumia zaidi madukani.


Nafuu nyengine ya maana ni ile ya kupunguzwa malipo ya bima ya afya.Hali hiyo itawanufaisha sio tuu waajiri na walipa kodi,bali pia watu waliostaafu na wengine wanaolipwa mishahara duni.Mpango huo utaigharimu serikali  kitita chengine cha yuro bilioni tisaa na hatua hiyo pia inastahiki kusifiwa na kupewa noti nzuri.Hata hivyo kimoja ni dhahiri nacho ni kwamba serikali haitamudu kujaza pengo la  mfumo wa huduma za jamii kwa muda mrefu.


Kishindo kinatokana na kinga ya serikali kwa mashirika ya kiuchumi.Suala hapo ni kumimina misaada ya fedha ili benki ziweze kutoa mikopo kwa wepesi zaidi-Sio lakini kwamba serikali inachangia kifedha katika mashirika hayo.Kwa namna hiyo kitisho cha kuona mashirika yakigeuka kua mali ya serikali kinatoweka,lakini ikiwa mashirika yatajikuta hali ya kuhitaji kuddhaminiwa,hali hiyo inaweza kua mzigo mkubwa kwa serikali.


Hatua nyengine ambayo haiwezi kupewa noti nzuri,ni ile ya kupewa kila mtoto mmoja yuro mia moja-pesa hizo hazitoshi kuchochea kiu cha kununua vitu madukani.Na zawadi za fedha zitakazotolewa kuzuwia magari ya zaidi ya miaka tisaa yasiendeshwe tena,itawafaidisha wenye viwanda vya magari tuu,na hapo hakuna ajuaye kama viwanda vitakavyofaidika ni vya kijerumani,kifaransa au pengine vya kijapan.


Licha ya yote hayo lakini mpango jumla uliopitishwa na serikali kuu ya muungano tunaweza kusema ni wa kijasiri-Ni wa kijasiri kwasababu ni wa kwanza mkubwa kiasi hicho katika historia ya baada ya vita nchini Ujerumani.