1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa gesi wa Ujerumani wasababisha mgawanyiko Ulaya

Grace Kabogo
5 Oktoba 2022

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameutetea mpango wa fedha wa euro bilioni 200 wa kuzuia ongezeko la bei ya gesi na kupunguza kodi ya mauzo ya mafuta.

https://p.dw.com/p/4HkqJ
Deutschland | Stahlwerk ThyssenKrupp in Duisburg
Picha: Rupert Oberhäuser/picture alliance

Akizungumza Jumanne na waandishi habari mjini Berlin, Scholz amesema mpango huo sio wa kipekee na kwamba ni sawa na hatua zinazochukuliwa na nchi nyingine kuwasaidia watumiaji na wafanyabiashara wakati wa mzozo wa nishati, kutokana na athari za kuongezeka kwa bei ya nishati.

''Lakini jukumu kubwa ni lazima bei ishuke na miundombinu ya nishati ya Ulaya iendelezwe kwa njia ambayo tutakuwa na uwezekano wa kuagiza gesi kutoka kwenye kila kona ya Ulaya, ili tusitegemee kuagiza kutoka Urusi,'' alifafanua Scholz.

Scholz autete mpango huo

Scholz ambaye alizungumza pia wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte mjini Berlin, amesema baadhi ya hatua zimekuwa katika mchakato wa muda mrefu na kwamba nchi nyingine zitafaidika kutokana na uwekezaji mkubwa kwenye mtambo wa kuchakata gesi asilia, LNG katika bandari za Ujerumani.

Amesema mpango huo sio tu kwa ajili ya Ujerumani, lakini kwa nchi nyingine jirani ikiwemo Jamhuri ya Czech, Slovakia, Austria na kwengineko. Baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zimekuwa na wasiwasi kwamba mpango huo unaweza kuzidisha mzozo wa nishati. 

Deutschland LNG Terminal Wilhelmshaven |
Kituo cha LNG kwenye mji wa Wilhelmshaven, UjerumaniPicha: Sina Schuldt/dpa/picture alliance

Kwa upande wake Rutte amesema Ujerumani ina kila haki ya kuchukua hatua hizo, lakini mara zote wanafanya mambo kwa pamoja kwa imani kamili kwamba wanashirikiana Ulaya yote kwa ajili ya soko thabiti la nishati. Hata hivyo, Scholz na Rutte wamesema ni mapema mno kufikiria kukopa upya kwa pamoja.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Christine Lindner, ambaye anatokea kwenye chama kinachozingatia zaidi sera za biashara cha Free Democratic, pia ameutetea mpango huo, akisema kulikuwa na hali ya kutoelewana. Akizungumza jana na mawaziri wenzake wa Umoja wa Ulaya huko Luxembourg, Lindner amewahakikishia mawaziri hao kwamba mpango huo wa fedha unalingana na ukubwa wa uchumi wa Ujerumani. Ujerumani inaongoza kwa kuwa na uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.

Kwa nini mpango huo una utata?

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema mpango huo hautokuwa na haki sawa na utawanufaisha zaidi wafanyabiashara wa Ujerumani katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya. Kamishna wa soko la ndani la Umoja wa Ulaya, Thierry Breton kutoka Ufaransa na kamishna wa umoja huo anayesimamia masuala ya uchumi, Paolo Gentiloni kutoka Italia wamesema mpango wa Ujerumani unazusha maswali mengi kuhusu haki. Wametoa wito wa kuwepo hatua pana za Umoja wa Ulaya kutumika ili kuzisaidia nchi.

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, ambayo inasimamia sera za kutoaminiana kote katika umoja huo, siku ya Jumatatu ilisema kwamba inafanya mazungumzo na Ujerumani kuhusu mpango huo wa fedha. Msemaji wa halmashauri hiyo amesema wamejizatiti kikamilifu kulinda viwango sawa na soko la pamoja, na kuzuia ushindani wenye madhara wa ruzuku.

(AFP, AP, DW)