Mpambano wa Ali na Foreman wakumbukwa | Magazetini | DW | 31.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Mpambano wa Ali na Foreman wakumbukwa

Magazeti ya Ujerumani wiki yameandika taarifa kuhusu ushindi wa Mohammed Ali dhidi ya George Foreman na pia kuhusu kifo cha mwanaspoti wa Afrika Kusini, Senzo Meyiwa.

Wiki hii imetimia miaka 40 tangu mabondia mashuhuri Mohammed Ali na George Foreman walipopambana katika uwanja wa kitaifa mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Rumble in the jungle. Ni mpambano ulioingia katika vitabu vya historia na Mohammed Ali aliwashangaza wengi kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Foreman ambaye mpaka wakati huo alikuwa hajawahi kushindwa ulingoni. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linakumbusha namna ambavyo dunia nzima ilijaa na shauku kabla ya mpambano huo.

Mpambano huu ulikuwa mchanganyiko wa maonesho na propaganda. Dikteta Mobutu Sesse Seko alikuwa miongoni mwa wale waliowezesha tukio hilo kufanyika nchini mwake. Kwa namna hiyo alijipatia umaarufu dunia nzima. Lilikuwa moja ya matukio yaliyofuatiliwa na watu wengi zaidi katika televisheni. Hapa Ujerumani, ilibidi watu waamke saa tisa usikui ili wasipitwe.

Makala hiyo inaendelea kuelezea namna ambavyo ushindi wa Mohammed Ali uliwahimiza maelfu kuwa mabondia. Mmojawao ni Biko Botowamungu kutoka jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Alipata uraia wa Austria na mwaka 1988 kushiriki katika michezo ya olimpiki. Safari yake ya kuwa mwanandondi ilianza siku alipushuhudia mpambano kati ya Foreman na Ali kwa macho akiwa kijana wa miaka 17.

Steinmeier na Fabius Nigeria

Frank-Walter Steinmeier alipoitembelea Nigeria

Frank-Walter Steinmeier alipoitembelea Nigeria

Magazeti ya Ujerumani yameandika pia kuhusu ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mwenzake Laurent Fabius wa Ufaransa, walioitembelea Nigeria wiki hii.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine Zeitung" linaeleza kwamba Fabius alikubali wazo la Steinmeier la kupeleka timu ya madaktari, wauguzi na maaskari kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwenye nchi zilizoathirika vibaya zaidi na janga la Ebola. Steinmeier alisema haelewi kwanini kuna kikosi cha Umoja wa Mataifa kinachopelekwa kwenye maeneo ya migogoro lakini hakuna kikosi cha kupelekwa kwenye nchi zenye majongwa ya mlipuko.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" nalo limechapisha taarifa kuhusu ziara ya Steinmeier na Fabius. Gazeti hilo linaeleleza kwamba ziara hiyo ilikuja wakati ambapo raia mmoja wa Ujerumani aliuliwa Nigeria na watu wasiojulikana. Hiyo ilitoa picha halisi kwa viongozi hao juu ya hali ya usalama nchini Niegria. Makundi ya kigaidi bado yanatishia amani.

"Meyiwa alikufa bila sababu"

Wiki hii kulikuwa pia na taarifa ya kuhuzinisha kutoka Afrika Kusini. Ni habari ya kuuliwa kwa kipa na nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Senzo Meyiwa

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine Zeitung" linasikitika kwamba Meyiwa aliuliwa kwa sababu tu walioivamia nyumba yake walikuwa wanataka simu yake ya mkononi. Gazeti hilo linaandika: Meyiwa alipigwa risasi na majambazi alipokuwa nyumbani kwa mchumba wake Kelly Khumalo. Kwa mujibu wa polisi, majambazi hao waliwataka watu wote saba waliokuwa ndani ya nyumba kutoa simu zao. Haifahamika iwapo Meyiwa alipigwa risasi kwa sababu aligoma kutoa simu au kwasababu alitaka kumkinga mpenzi wake asilengwe.

Senzo Meyiwa alikuwa kipa na nahodha wa timu ya taifa

Senzo Meyiwa alikuwa kipa na nahodha wa timu ya taifa

Makala hiyo inaeleza kwamba kifo cha Meyiwa kimezua upya mjadala kuhusu umiliki wa silaha Afrika Kusini. Tukio hili linakuja siku chache baada ya mwanariadha Oscar Pistorius kufungwa jela kwa sababu ya kumuua mpenzi wake kwa bunduki.

Katika kurasa za "Süddeutsche Zeitung" tunakutana pia na habari ya kifo cha Meyiwa. Gazeti hilo linasema kuwa kifo hiki kimewagusa wengi kwa sababu Meyiwa hakuwa kipa tu, alikuwa pia nahodha na mmoja wa nyota wa michezo barani Afrika.

Katika makala hii inakumbushwa kwamba Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa mauaji duniani. Kila mwaka wanauliwa watu 17,000. Hiyo ni sawa na mauaji 50 kwa siku! Ni katika visa vichache tu ambapo muuaji anakamatwa na kushtakiwa. Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema anashindwa kuelezea kushtushwa kwake na tukio hili, huku rais wa shirikisho la kandanda duniani, Sepp Blatter, akisema kuwa Meyiwa alikufa bila sababu.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman