1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morsi ahukumiwa Kifo

16 Mei 2015

Rais aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohammed Morsi ambaye tayari anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la uchochezi wa ghasia dhidi ya waandamanaji,amehukumiwa kifo

https://p.dw.com/p/1FQcX
Rais wa Zamani wa Misri Mohammed Morsi
Rais wa Zamani wa Misri Mohammed MorsiPicha: picture alliance/AP Photo/T. el-Gabbas

Morsi amehukumiwa kifo kwa kosa la udukuzi pamoja na kufanikisha uvunjwaji wa jela karibu miaka miwili baada ya kuangushwa kwake madarakani.

Morsi ambaye ni rais wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini Misri alipinduliwa madarakani na mkuu wa jeshi ambaye sasa ni rais wa nchi hiyo,Abdel Fatah al Sisi mnamo mwezi Julai mwaka 2013. Morsi aliondolewa madarakani baada ya kushuhudiwa maandamano makubwa katika mitaa ya Misri ya wananchi waliotaka ajiuzulu madarakani mwaka mmoja baada ya kutwaa madaraka.

Maandamano mjini Kairo 24.01.2015
Maandamano mjini Kairo 24.01.2015Picha: Mohamed El-Shaed/AFP/Getty Images

Kuondolewa kwake madarakani kulichochea hatua za kuandamwa na serikali kundi la Udungu wa Kiislamu ambapo mamia ya watu waliuwawa na maelfu wakatiwa jela.

Washtakiwa katika kesi zote zilizosikilizwa leo Jumamosi (16.05.2015) walifikishwa mahakamani na kusimamishwa kizimbani kabla ya kutolewa hukumu.Washtakiwa walisikika wakisema ni wanamapinduzi huru na wataendelea na maandamano.

Mosri alifikishwa mahakani sambamba na kiongozi wa Udugu wa kiislamu Mahmud Badie aliyefikishwa mahakamani akiwa amevalishwa sare nyekundu ambayo kawaida huvishwa watuhumiwa waliohukumiwa kifo.

Mashirika ya haki za binadamu yanaushutumu utawala wa Sisi ambao kwa kiasi kikubwa unaungwa mkono na wamisri waliochoshwa na miaka chungunzima ya misukosuko ya kisiasa na mivutano,kwa kutumia taasisi za sheria kama chombo cha kuwakandamiza wapinzani.

Rais wa sasa wa Misri Abdel Fatah-al Sisi
Rais wa sasa wa Misri Abdel Fatah-al SisiPicha: Reuters/Dalsh

Morsi alihukumiwa kifungo cha miaka 20 mwezi uliopita kwa kosa la kuchochea ghasia dhidi ya waandamanaji mwaka 2012 wakati alipokuwa madarakani,hukumu ambayo shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu,Amnesty International limeilaani na kuitaka kama kitendo kinachokandamiza haki.

Leo Jumamosi Morsi na wengine 130 ikiwemo wanachama wa kundi la Hamas la palestina na Hezbollah la Lebanon walifikishwa mahakamani kusikiliza kesi na hukumu dhidi yao wakituhumiwa kwa makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutoroka jela na kuwashambulia polisi wakati wa vuguvugu la kudai demokrasia dhidi ya kiongozi wa muda mrefu Misri Hosni Mubarak.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sudi Mnette