1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogherini ziarani Uturuki

Mohamed Dahman8 Desemba 2014

Mkuu mpya wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kukutana na viongozi wa Uturuki kwa mazungumzo yanayotarajiwa kulenga vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria

https://p.dw.com/p/1E10p
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini.
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini.Picha: JOHN THYS/AFP/Getty Images

Serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zina wasi wasi juu ya uwezekano wa kuenea kwa mzozo huo wa Syria na uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya raia wa Ulaya wanaorudi nyumbani baada ya kupambana bega kwa bega na majihadi nchini Iraq na Syria.

Mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Ulaya ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mzozo wa Syria litakuwa mojawapo ya suala kuu katika agenda ya ziara ya Mogherini inayoanza Jumatatu (08.12.2014).

Uturuki iko kwenye shinikizo la kuzuwiya wapiganaji wanaokwenda kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu kwa kupitia mipaka yake ambayo imekuwa ndio njia kuu kati ya Ulaya na maeneo yanayodhibitiwa na kundi la IS.

Mogherini ambaye katika ziara hiyo anaandamana na Kamishna anayeshughulikia suala la kutanuka kwa Umoja wa Ulaya Johannes Hahn na Kamishna wa Misaada ya Kibinaadamu Christos Stylianders anatazamiwa kukutana na Rais Recep Tayyip Erdogan,Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu na Waziri wa mambo ya nje Meviut Cavusoglu mjini Ankara.

Umuhimu wa Uturuki

Mogherini waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Italia ambaye amechukuwa wadhifa huo wa mkuu wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya hapo Novemba Mosi pia anatarajiwa kutembelea kambi za wakimbizi zilioko kwenye mpaka wa kusini wa Uturuki hapo Jumanne.

Kasri jipya la Rais mjini Ankara Uturuki.
Kasri jipya la Rais mjini Ankara Uturuki.Picha: picture-alliance/dpa/Stringer

Umoja wa Ulaya umesema katika taarifa kwamba ziara hiyo inayofanywa kwa pamoja na viongozi wa Umoja wa Ulaya inaonyesha umuhimu wa Uturuki ikiwa kama nchi inayogombea uwanachama wa kujiunga na Umoja wa Ulaya na kama mshirika muhimu na jirani kwa kuzingatia eneo ilioko kuwa la mkakati na kuwa na uchumi wenye nguvu.

Umoja wa Ulaya umesema hiyo pia ni ishara ya wazi ya nia yao na kuwa tayari kwao kuimarisha mawasiliano katika ngazi yote ya uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kukidhi umuhimu mkubwa wa uhusiano wao.

Kujiunga na Umoja wa Ulaya

Uturuki ambalo ni taifa lenye nguvu la Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika kanda hiyo haikupiga hatua kubwa katika mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya tokea yalipoanza rasmi hapo mwaka 2005.

Bendera za Umoja wa Ulaya.
Bendera za Umoja wa Ulaya.Picha: Georges Gobet/AFP/Getty Images

Mazungumzo hayo yamekwama kutokana na vizingiti mbali mbali ikiwa ni pamoja na mzozo wa ardhi na nchi mwanachama Cyprus na upinzani kutoka vigogo vya Umoja wa Ulaya Ujerumani na Ufaransa.

Serikali ya Uturuki pia inashutumiwa na Umoja wa Ulaya kwa rekodi yake ya haki za binaadamu huku baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zikiwa na mashaka ya kuipa uwanachama nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Waislamu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman