1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mapigano mapya yazuka wawili wauawa

29 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUr

Raia wawili wameuawa nchini Somalia huku ghasia zikiripotiwa kuendelea katika mji mkuu.Wapiganaji waliwaua watu wawili katika mkoa wa Kusini wa Medina katika ghasia za usiku kucha.Majeshi ya serikali yalipambana na wapiganaji kwenye eneo la kaskazini la Suqaholaha kwa siku ya pili japo idadi kamili ya majeruhi haijulikani.

Watu saba waliuawa jana usiku mjini Mogadishu ambako wapiganaji wa mahakama za kiislamu wanaongeza nguvu mashambulizi yao ya kupambana na jeshi la serikali linaloshirikiana na majeshi ya Ethiopia kuwafurusha.

Wakati huohuo serikali ya muda ya Somalia inafanya mkutano wa maridhiano ya kitaifa mjini Mogadishu unaolenga kuleta pamoja koo zinazozozana vilevile kuimarisha uongozi wa rais Abdullahi Yusuf Ahmed nchini humo.Hata hivyo wapiganaji wa mahakama za kiislamu vilevile wawikilishi wa ukoo wa Hawiye ulio na ushawishi mkubwa wanasusia kikao hicho.

Somalia imekuwa bila serikali tangu mwaka 91 baada ya kungolewa madarakani kwa Mohamed Siad Barre.