1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogadishu.Ethiopea yashambulia uwanja wa ndege Mogadishu

25 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCg8

Ndege za kivita za Ethiopea zimeushambulia kwa mabomu uwanja wa ndege wa Mogadishu katika mji mkuu wa Somalia , yakiwa ni mashambulizi dhahiri ya Ethiopea, dhidi ya muungano wa mahakama za kiislam.

Katika mashambulizi hayo imeripotiwa kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa, ikiwa ni pamoja na majengo kadhaa yanayotumiwa na muungano wa mahakama hizo za kiislam.

Serikali ya Ethiopea imethibitsha kufayika kwa shambulizi hilo ambapo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ethiopea Solomon Abebe amesema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa na nia ya kuzua misafara isiyoruhusiwa.

Msemaji huyo amesema kuwa ilibainika kuwa wapiganaji wa kihafidhina walikuwa uwanjani hapo kusafirishwa.

Pia kuna habari ya kwamba ndege za Ethiopea ziliushambulia kwa mabomu uwanja wa ndege wa Belidogle uliyoko kiasi cha kilomita 90 kusini magharibi mwa Mogadishu, ambako wapiganaji wa muungano wa mahakama za kiislam ndiko wanakohifadhi mahitaji yao.

Mashambulizi hayo yamekuja siku moja tu babada ya Waziri Mkuu wa Ethiopea, Meles Zenawi kukiri hadharani kuwa majeshi yake yanaisadia serikali ya mpito ya Somalia kupambana na muungano huo wa mahakama za kiislam.

Zenawi alisema kuwa Ethiopea imelazimika kuingia vitani kulinda utawala wake dhidi ya kile alichokiita magaidi na maadui wa Ethiopea.

Ndege za kivita za Ethiopea ziliangusha mabomu leo alfajiri katika uwanja wa kimataifa wa Mogadishu, ambao ulifungiliwa hivi karibuni baada ya majeshi ya muungano wa mahakama za kiislam kuutwaa.

Mashambulizi hayo ya anga yamefanyika saa chache baada ya majeshi ya serikali ya mpito yanayoungwa mkono na Ethiopea kufanikiwa kuuteka mji wa Belet Weyne uliyo katika mpaka wa Somalia na Ethiopea.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati pande hizo, huku kila upande ukidai kuua mamia ya maadui.

Mapigano makali yalianza jumatano iliyopita baada ya muda wa mwisho uliyowekwa na muungano wa mahakama za kiislam kwa majeshi ya Ethiopea kuondoka katika ardhi ya Somalia

Umoja wa Ulaya umelaani hali hiyo ya mapigano na fujo huko Somalia na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.

Wataalam wa masuala ya kivita wanakadiria kuwa Ethiopea ina kiasi cha wanajeshi elfu 20 nchini Somalia , huku hasimu wake mkubwa Eritrea ikiwa na askari kiasi cha elfu 2 wanaounga mkono muungano wa mahakama za kiislam.