1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Serikali ya Somalia itatumia sheria ya kijeshi kudhibiti nchi nzima.

29 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfK

Waziri Mkuu wa Somalia, Ali Mohamed Gedi amesema bunge litatangaza muda wa kutumiwa sheria ya kijeshi ili kudumisha udhibiti wa nchi hiyo.

Ali Gedi ametangaza hayo baada ya majeshi ya serikali yakisaidiwa na Ethiopia kuuteka mji wa Mogadishu uliokuwa ukisimamiwa na wanamgambo wa Kiislamu.

Mji wa Mogadishu umetekwa baada ya mapambano ya siku kumi kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa kiislamu ambao wamekuwa wakisimamia eneo kubwa la nchi hiyo tangu mwezi Juni.

Waziri wa habari wa Somalia alielezea jinsi hali ya mambo ilivyokuwa baada ya majeshi ya serikali kuteka mji wa Mogadishu:

"Serikali ya Somalia inaudhibiti mji wa Mogadishu. Waziri Mkuu Ali Gedi amewasili mjini humo. Naibu waziri Mkuu Hussein Aideed na naibu waziri wa ulinzi Salad Jelle walikuwa wametangulia wakiandamana na mawaziri waliokuwa wakishauriana na wakuu wa koo kuhusu kuanzishwa kwa utawala mpya mjini Mogadishu"

Wanamgambo wa Kiislamu wamekiri kwamba wameondoka mjini humo lakini wakasema wataanza tena mapigano kujaribu kuyaondoa majeshi ya Ethiopia.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa unapanga kurejelea safari za ndege za kutoa misaada katika maeneo ya kati na kusini ambayo yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mzozo huo pamoja na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni.

Kwengineko watu takriban kumi na saba wamefariki baada ya mashua mbili walizokuwa wakisafiria kutokea Somalia kuzama katika pwani ya Yemen.

Watu wengine kiasi cha mia moja na arobaini wametoweka kwenye mkasa huo uliotokea kwenye ghuba ya Aden.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi, UNHCR, limesema mashua hizo mbili zilikuwa zikiwasafirisha raia wa kisomali na Ethiopia wanaokimbia mapambano yanayoendelea kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa mahakama za Kiislamu.

Askari polisi wa Yemen wanaoshika doria katika eneo la pwani wamesema wafanyikazi wa huduma za uokoaji wangali wakitafuta manusura.