1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Mkutano wa usuluhishi wa kitaifa Somalia

23 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPb

Rais Abdulahi Yusuf wa Somalia amesema hapo jana ataandaa mkutano wa usuluhishi wa kitaifa hivi karibuni ambao utakuwa wazi kuhudhuriwa na makabila yote kwenye nchi hiyo ambayo bado ingali inakabiliwa na umwagaji damu kufuatia vita vya mwezi wa Desemba.

Katika umwagaji damu huo unaozidi kupamba moto katika mji mkuu wa Mogadishu na viunga vyake makombora ya mizinga yalishambulia uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Mogadishu hapo jana na wanajeshi wawili wa serikali waliuwawa katika mapambano na wapiganaji wenye silaha.

Yusuf amekaririwa akiliambia shirika la habari la Uingereza Reuters katika mahojiano wakati akiwa ziarani mjini London kwamba wanakusudia kuanza mkutano huo katika kipindi cha wiki mbili tatu zijazo na kwamba wataanzia na ngazi ya taifa hadi kufikia ngazi ya vijijijini.

Yusuf amesema watu wao wamepigana vikali, wamekuwa wakichinjana wenyewe kwa wenyewe na kwamba sasa inabidi wajadili jinsi ya kusahao na kusamehe.

Serikali ya mpito ya Somalia ikisaidiwa na ndege za kivita za Ethiopia, vifaru na wanajeshi imeutimuwa muungano wa mahkama za Kiislam kutoka Mogadishu na kusini mwa nchi hiyo hapo mwezi wa Desemba mwaka jana.