1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Marekani yashambulia tena Somalia

25 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYD

Marekani imefanya shambulio la pili la anga nchini Somalia wakati mjumbe mwandamizi wa serikali ya Marekani Afrika Mashariki akikutana na kiongozi wa Kiislam alieangushwa nchini Somalia kushinikiza usuluhishi na serikali ya nchi hiyo.

Shambulio hilo jipya la anga limekuja wiki mbili baada ya ndege za AC-130 za Marekani kuuwa kile Marekani ilichosema kuwa wapiganaji wanane wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda ambao walikuwa wamejificha miongoni mwa wapiganaji wa Kiislam wa Somali waliokuwa wametimuliwa hadi kusini kabisa kwa mwa nchi hiyo na vikosi vya Ethiopia na vile vya serikali ya mpito ya Somalia.

Mojawapo wa maafisa wa serikali ya Marekani amesema mashambulizi ya wiki hii yalilenga kundi la wanamgambo wa Muungano wa Mahkama ya Kiislam wakati duru nyengine zinasema mashambulizi hayo yalilenga wanachama wa Al Qaeda.

Balozi wa Marekani nchini Kenya Michael Ranneberger amekutana na kiongozi wa Muungano wa Mahkama za Kiislam Sheikh Sharif Ahmed ambaye anashikiliwa na maafisa usalama wa Kenya kwenye hoteli moja mjini Nairobi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema lengo ni kutaka kujuwa nia za Sheikh huyo ili kushajiisha kile inachotaka Marekani mazungumzo na ushirikiano kati ya serikali ya mpito ya Somalia na Waislamu wa msimamo wa wastani.