1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mo Ibrahim: Mapinduzi ya kijeshi yameshamiri Afrika

Sylvia Mwehozi
25 Januari 2023

Ripoti mpya iliyotolewa siku ya Jumatano juu ya utawala bora barani afrika inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya bara hilo imeporomoka katika nyanja za usalama na demokrasia kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita

https://p.dw.com/p/4MguX
Burkina Faso | PK Ibrahim Traore
Picha: AA/picture alliance

Kwa mujibu wa faharasa ya utawala bora iliyokusanywa na Wakfu wa Mo Ibrahim, kurudi nyuma kwa demokrasia sasa kunatishia kurejesha nyuma maendeleo yaliyopatikana kwa miongo kadhaa barani Afrika. Wakfu huo, umeorodhesha jumla ya mapinduzi 23 yaliyofanikiwa na yale yaliyoshindwa huku ikiyataja mapinduzi 8 kutokea tangu mwaka 2019.

Mo Ibrahim, ukuwaji wa uchumi na utawala mbaya Afrika

Nchi ya Mali na jirani yake Burkina Faso zimeshuhudia mapinduzi ya mara mbili katika kipindi hicho na hivyo kudhoofisha zaidi kanda hiyo ya ulimwengu ambayo tayari inakabiliwa na mzozo wa wanamgambo wa Kiislamu. Bilionea wa Uingereza Mo Ibrahim ambaye ni mzaliwa wa Sudan anayetumia utajiri wake katika kukuza demokrasia na uwajibikaji wa kisiasa barani afrika amesema kuwa "hali hii ya mapinduzi ya kijeshi ambayo ilikuwa ya kawaida katika miaka ya 80, sasa inaonekana tena kuwa mtindo katika baadhi ya maeneo ya Afrika".

Mo Ibrahim: 'Africa has no voice' in the climate debate
Bilionea Mo IbrahimPicha: DW

Waandishi wa ripoti hiyo pia wamegundua kuenea kwa matatizo ya kiusalama kwa ujumla. Katika muongo mmoja uliopita, karibu asilimia 70 ya waafrika walishuhudia hali ya usalama na utawala wa sheria vikiporomoka katika nchi zao. Zaidi ya nchi 30 zimeshuka katika kipengele hicho kwa mujibu wa faharasa hiyo. Sudan Kusini iko mkiani ikifuatiwa na Somalia, Eritrea, Congo, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Burundi, Libya na Guinea ya Ikweta. Nchi tano zilizofanya vyema katika utawala bora ni Mauritius, visiwa vya Ushelisheli, Tunisia, Cape Verde na Botswana. Ripoti hiyo pia inadokeza kwamba Gambia na visiwa vya Ushelisheli na baadhi ya nchi "zinapinga mwelekeo wa bara" na kutaja maendeleo mapana katika masuala ya wanawake.Mo Ibrahim: Nchi tajiri ziache kujiwekea chanjo ya COVID-19

Udhalimu wa serikali dhidi ya raia na machafuko ya kisiasa vimeongezeka kote Afrika tangu kuzuka kwa janga la Covid-19 huku serikali hizo zikitajwa kutumia vizuizi vya kukabiliana na ugonjwa huo kwa ajili ya kukandamiza wapinzani. "Ingawa hali hii imekuwepo hata kabla ya janga, lakini mwelekeo huo wa kupinga demokrasia umechochewa na kuanzishwa kwa vizuizi vikali na hali za dharura ambazo zimeendelea kurefushwa", ilisema ripoti hiyo.

Bilionea Mo Ibrahim anasema kwamba nchi za kiafrika lazima zipigane dhidi ya kushamiri kwa tawala za kiimla ambazo ni matokeo ya mkururo wa mapinduzi ya kijeshi na ukandamizaji dhidi ya raia. Utafiti huo, ambao ulipima maendeleo katika muongo mmoja uliopita katika mada tofauti kuanzia afya na elimu hadi usalama na utawala wa sheria, uligundua kuwa utawala kwa ujumla umeshuka tangu mwaka 2019.

Faharasa hiyo pia imeshuhudia maendeleo katika baadhi ya vipengele vya uchumi, elimu na usawa wa kijinsia. Hata hivyo, ripoti hiyo ilichambua taarifa hizo hadi mwisho wa mwaka 2012 na kwahiyo haikuzingatia athari kamili za janga la ulimwengu la Covid-19. Maeneo mengine yanayoonekana kupiga hatua ni katika ujenzi wa miundombinu, kuimarika kwa usawa kwa wanawake pamoja na uboreshwaji wa upatikanaji wa huduma za afya, elimu na mazingira tangu mwaka 2012.