1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnyamar yaruhusu msaada kutoka Marekani

Mwakideu, Alex8 Mei 2008

Serikali na wananchi kadhaa walipata habari za kutokea kwa kimbunga cha Nargis mapema kabla hakijatokea

https://p.dw.com/p/DwbX
Mti ulioanguka unazuia usafirishaji mjini YangunPicha: picture-alliance / dpa

Kufuatia shutuma za kimataifa hatimaye Miyanmar imeruhusu angalau ndege moja ya Marekani ya msaada itue nchini humo ili mamilioni ya wananchi walioathirika na kimbunga cha Nargis waweze kusaidika.


Huku idadi ya waliofariki na waliopotea ikihofiwa kupita watu 60, 000 Miyanmar imesema ilitoa onyo la kutokea kwa kimbunga cha Nargis siku sita kabla hakijatokea.


Kauli ya serikali ya Miyanmar ya kuchelewa kuruhusu misaada ya kimataifa nchini humo imezua hisia kali miongoni mwa nchi mbali mbali na kuwaweka mamilioni ya wananchi walioachwa bila makao na wanaohitaji maji na chakula katika hali mbaya zaidi.


Misaada ya kimataifa inayowasili mjini Yangun haiwezi kusambazwa vyema hadi katika jimbo la Irrawaddy Delta lililoathirika zaidi na kimbunga cha Nargis. Jimbo hilo lililoko kusini mwa Miyanmar lilifunikwa na maji katika kimbunga hicho kilichotokea jumamosi.


Msemaji wa Umoja wa Mataifa Richard Horsey anasema kuna takriban watu milioni moja wanaohitaji msaada katika jimbo hilo na kufika katika eneo hilo kunahitaji madau, elikopta na pia malori.


Horsey anaeongea kwa niaba ya afisi ya misaada ya Umoja wa Mataifa OCHA anasema takriban kilomita 5000 mraba ya eneo hilo imefunikwa na maji "kwa jumla eneo lote la chini la Delta liko chini ya maji. Hayo yamedhihirika kutokana na picha mpya kabisa za satilaiti. Na hii inaonyesha kweli changamoto zinazokabili kikosi hiki kinapojaribu kufikisha misaada ya dharura kwa umma unaouhitaji" Horsey alisema.


Amesema licha ya meli kadhaa za misaada kuwasili nchini Miyanmar, hakuna ndege yoyote imetua mjini Yangun kwa shughuli za kusafirisha misaada hiyo.


Msemaji wa shirika la watoto la UNICEF Shantha Bloemen amesema shirika hilo linatarajia kusambaza msaada wake kwa kutumia bara bara lakini linahitaji shirika la msalaba mwekundu la Miyanmar kwa shughuli za kuusafirisha.


Horsey anasema iwapo hakutakuwa na msaada wa dharura basi idadi ya watu waliofariki ambayo inakadiriwa kufika 23 elfu huenda ikaongezeka zaidi.


Ameongezea kwamba maelfu ya miili inayooza katika maji nchini humo huenda ikaeneza magonjwa kwa manusura na kusababisha vifo zaidi.


Marekani na Ufaransa zimejitolea kutuma meli za misaada zilizoko karibu na Miyanmar lakini maombi yao hayajajibiwa.


Afisi ya misaada ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema baadhi ya wataalamu wake walitarajiwa kutoka Italy jana na kuja Miyanmar wakiwa na tani 25 za msaada lakini bado hawajaanza safari yao.


Shirika la chakula duniani WFP nalo limesema linataka kutuma ndege kadhaa zilizojaa biskuti zenye afya na misaada mingine ya dharura lakini bado hawajapewa idhini ya kutua mjini Yangun.


Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa tayari limetumana tani 22 za misaada ambayo ipo mpakani mwa Tailand na Miyanmar ikisuburi kuruhusiwa nchini humo.


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na waziri wa nchi za kigeni wa Marekani Condoleezza Rice wametoa wito kwa nchi hiyo isiyokuwa na imani na jamii ya kimataifa kuruhusu misaada iingiizwe ndani.


Msemaji katika wizara ya nchi za nje nchini China Qin Gang amesema hasara iliyosababishwa na kimbunga cha Nargis ni kubwa sana kwa Miyanmar kuweza kuikabili peke yake.


Qin amesema China imeamua kutuma msaada mwengine wa dola milioni 4 na laki 3 kando na ule wa dola milioni moja ambao ilitangaza kutuma hapo juzi.


Hata hivyo Gang ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuheshimu serikali ya Miyanmar.


Shirika la utabiri wa hali ya hewa ulimwenguni WMO limesema Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Miyanmar inadai ilitoa onyo la kutokea kwa kimbunga cha Nargis siku sita kabla hakijatokea.


Taarifa kutoka kwa shirika hilo inasema imepokea habari kutoka Miyanmar zinazosema kwamba onyo lilitolewa tarehe 27 aprili na serikali ya Miyanmar ilitahadharishwa tarehe 29 mwezi huo huo.


Vyombo vya habari nchini humo vilipokea habari hizo mei mosi na magazeti yalizichapisha tarehe 2 mei.


Wakaazi wa Yangun wamedhibitisha kuzisoma taarifa hizo za tahadhari katika magazeti lakini wanahofia kwamba wakaazi wengine wa vijijini hawangeweza kuyaona magazeti hayo.


Serikali ya kijeshi ya Miyanmar imeshutumiwa vikali na jamii ya kimataifa hususan mkewe Rais wa Marekani Laura Bush kwa kukosa kutoa tahadhari ya kimbunga cha Nargis.