1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Ujasusi wa Rwanda akamatwa mjini London

Admin.WagnerD23 Juni 2015

Ubalozi wa Uingereza nchini Rwanda umesema Emmanuel Karenzi Karake ambaye ni mkuu wa ujasusi amekamatwa kutokana na waranti wa Jaji wa Uhispania.

https://p.dw.com/p/1Fm3B

Taarifa ya Ubalozi huo wa Uingereza mjini Kigali ilisema kwamba kukamatwa Emmanuel Karenzi Karake mwenye umri wa miaka 54 na mshirika wa karibu wa rais Paul Kagame, kunatokana na uhalali wa kisheria kufuati waranti wa Ulaya.

Hatua hiyo imezusha malalamiko makali kutoka kwa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo ambaye kupitia mtanado wake wa Twitter leo alisema mshikamano wa nchi za magharibi katika kuwadhalilisha waafrika, si jambo linalokubalika na kuongeza kwamba hatua hiyo ya kumkamata mkuu huyo wa ujasusi na vyombo vya usalama wa taifa, ni tukio la kusikitisha.

Kukamatwa kwa mkuu huyo wa ujasusi kunatokana na mashtaka yaliowasilishwa 2008 na jaji wa uhispania Fernando Andreu Merelles anayewatuhumu wanajeshi na viongozi wa kisiasa 40 wa Rwanda Patriotic Front-RPF, kundi la waasi wa zamani lililotwaa madaraka 1994 na kuzuwia mauaji, kwamba walifanya mauaji ya kulipiza kisasi mnamo miaka iliofuatia mauaji ya kimbari. Jaji huyo amewafungulia mashtaka maafisa hao ya mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binaadamu na ugaidi kuhusiana na vifo vya mamia kwa maelfu ya raia wakiwemo raia wanane wa Uhispania ambao walikuweko Rwanda kwa shughuli za misaada ya kibinaadamu. Wakati huo serikali ya Rwanda ilikanusha tuhuma hizo na kusema hazina msingi hata kidogo.

Kwa muda mrefu Rwanda imezishutumu nchi za magharibi na nyenginezo kwa kile ilichosema hazikuwajibika kuzuwia mauaji ya kimbari na baadae kushindwa kuchukuwa hatua za ziada kuwaangamiza wauaji wa kundi la waasi wa Kihutu la FDLR.

Wapiganaji wa kundi hilo waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, walihusika katika mauaji ya karibu Watutsi na Wahutu wal msimamo wa wastani 800,000 mwaka 1994.

Kisa cha kukamatwa mjini London kwa Mkuu wa ujausi na vyombo vya usalama wa serikali ya sasa ya Rwanda , sasa kimeibuwa mvutano mwengine kati ya Rwanda na Uingereza ambazo uhusiano wao umekuwa si mzuri. Pamoja na hayo waziri wa sheria wa Rwanda Johnston Busingye amesema nchi hizo mbili zinazungumza kulitafutia ufumbuzi suala hilo, lakini amesisitiza kwamba waranti wa kumtia nguvuni uliotolewa na Uhispania hauna msingi kisheria na una malengo ya kisiasa .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, ap

Mhariri:Yusuf Saumu