Mkuu wa NATO aonya kuhusu Urusi kuivamia Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkuu wa NATO aonya kuhusu Urusi kuivamia Ukraine

Kamanda mkuu wa NATO akisema ana “wasiwasi mkubwa” kuwa kuendelea kukusanyika wanajeshi la Urusi katika eneo la Crimea kunaweza kutumiwa kama chanzo cha mashambulizi katika kanda nzima ya Bahari Nyeusi.

Jeshi la Ukraine limesema leo kuwa raia wawili wameuawa katika makabiliano ya karibuni mashariki mwa Ukraine, wakati waangalizi wa kimataifa wanaofuatilia mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi wanaoiunga mkono Urusi wakiripoti kushambuliwa.

Serikali ya mpya ya Ukraine wiki hii ilielezea nia yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, jambo lililoikasirisha Urusi ambayo inapinga kabisa upanuzi wa taasisi za magharibi katika kile inachokizingatia kuwa ni himaya yake.

Raia wa Ukraine awali hawakutilia maanani sana uwanachama wa NATO lakini kumekuwa na mabadiliko makubwa ya maoni ya umma tangu Urusi ilipoanza kujihusisha na vuguvugu la uasi la kutaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, ambalo kufikia sasa limesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,300 tangu mwezi Aprili mwaka huu.

Uchunguzi wa maoni wa karibuni umeonyesha kuwa asilimia 51 ya raia wa Ukraine wanaunga mkono uwanachama wa NATO, kutoka asilimia 20 mwaka mmoja uliopita.

Ukraine Besuch U.S. General Philip Breedlove 26.11.2014

Jenerali wa Marekani Philip Breedlove anayeongoza kikosi cha NATO, barani Ulaya

Hata hivyo uwezekano wa kuwa mwanachama wa NATO unasalia kuwa mdogo sana, kwa sababu Ukraine haina mipaka salama na wanachama wa sasa wanahofia kuichokoza zaidi Urusi.

Katika mji wa Donetsk unaodhibitiwa na waasi, mashariki mwa Ukraine, maisha ya watu wa kawaida yanaendelea kuwa magumu huku mitambo ya kutoa pesa ikiishiwa fedha baada ya benki kuu ya Ukraine kuamuru kufungwa mfumo wa mabenki katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Kamanda mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jenerali wa Marekani Philip Breedlove amesema ana “wasiwasi mkubwa” kuwa kuendelea kukusanyika kwa jeshi la Urusi katika eneo la Crimea kunaweza kutumiwa kama chanzo cha mashambulizi katika kanda nzima ya Bahari Nyeusi.

Matamshi ya Breedlove, yamekuja wakati kukiwa na hofu nchini Ukraine kuwa waasi wanaoungwa mkono na Urusi watajaribu kunyakua ardhi zaidi mashariki mwa Ukraine ili kuweka ukanda wa ardhi kuelekea jimbo la Crimea, ambalo Urusi ililifanya kuwa sehemu ya himaya yake mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Lakini Rais wa Urusi Vladmir Putin anasema Urusi siyo kitisho kwa yeyote na itafanya kila liwezekanalo kuilinda mipaka yake. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa imepeleka ndege 14 za kijeshi katika eneo la Crimea kama sehemu ya kikosi chake kilichoko katika rasi hiyo.

Breedlove pia amerudia shutuma kuwa majeshi ya Urusi yako ndani ya mashariki mwa Ukraine “yakitoa mafunzo, na kuwapa silaha” waasi wanaopigana katika eneo hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com