1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa NATO aonya EU haiwezi kuilinda Ulaya peke yake

Saleh Mwanamilongo
4 Machi 2021

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameonya kuwa EU haiwezi kuwalinda raia wake peke yake bila msaada wa muungano huo wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/3qDby
NATO Gipfel in Brüssel Mazedonien Einladung zu Beitrittsgesprächen
Picha: Reuters/D. Zammit Lupi

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakishinikiza jumuiya yao kujenga "uhuru zaidi wa kimkakati", hatua ambayo baadhi wanaiona kama inaweka ushindani kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Lakini Stoltenberg, amesema mataifa ya Umoja wa Ulaya ambayo yalikuwa wanachama wa NATO yanaunda tu moja juu ya tano ya bajeti ya jumla ya matumizi ya ulinzi ambayo inazilinda fukwe za Ulaya.

Amesema Umoja wa Ulaya hauwezi kuilinda Ulaya peke yake, akisema zaidi ya asilimia 90 ya raia wa Umoja wa Ulaya wanaishi katika nchi ya NATO. Lakini wanachama wa Umoja wa Ulaya wanatoa tu asilimia 20 ya bajeti ya ulinzi ya NATO.

''Sio tu suala la kifedha pekee. Ni suala pia la kijiografia. Iceland na Norway, huko kaskazini mwa Ulaya ni milango ya kufikia bahari ya Arctic. Kusini Uturiki inapakana na Syria na Irak na upande wa magharibi Marekani,Canada na Uingereza vinafungamana na bahari ya Atlantiki'' alisema Stoltenberg.

Joe Biden na sera mpya ya NATO

Baadhi ya viongozi wa Ulaya, akiwemo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, wakihoji ikiwa mkakati wa jumuiya ya NATO umefeli duniani bada ya vita baridi.

Lakini Wengine akiwemo Stoltengerg, wameona uchaguzi wa Joe Biden kama rais wa Marekani, kama fursa ya kuboresha upya mahusiano baina ya nchi wanachama ambayo yalizorota chini ya uongozi wa Donald Trump.

Halmashauri Kuu ya Ulaya inataka kuchukua jukumu imara la kijiografia, kwa kuidhinisha sera za kigeni zenye uthubutu zaidi na kuimarisha sekta za ulinzi barani Ulaya.