1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa IAEA aonya atajiuzulu ikiwa Iran itavamiwa kijeshi

21 Juni 2008

-

https://p.dw.com/p/ENoz

DUBAI

Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya nishati ya Nuklia la IAEA Mohammed El Baradei ameonya kwamba atajiuzulu endapo nguvu za kijeshi zitatumika dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wa kinuklia wa nchi hiyo.Akizungumza hapo jana katika mahojiano na televisheni ya kiarabu ya Al Arabiya mkuu huyo amesema hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran katika wakati kama huu italigeuza eneo zima katika moto mkubwa.

Wakati huohuo Marekani imesema itaendelea kuunga mkono suluhisho la kidiplomasia juu ya mzozo na Iran.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Sean McCormack amewaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba Marekani itaendelea kutumaini kuwa Iran itashawishika kukomesha shughuli zake za kurutubisha madini ya Uranium kama ilivyotakiwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa.Kwa upande mwingine amekataa kuzungumzia chochote juu ya ripoti kwamba wanajeshi wa angani wa Israel wamekuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi ambayo yanaaminika ni ya kujiandaa na uwezekano wa kuvamia vinu vya kinuklia vya Iran.Gazeti la New York Times la Marekani liliripoti hivi karibuni kwamba ndege zaidi ya 100 za kijeshi za Israel zimekuwa zikifanya mazoezi katika eneo la bahari ya Mediterranean na Ugiriki mapema mwezi huu.Marekani na nchi nyingine za magharibi zinahofia kuwa Iran inataka kutengeneza silaha za Kinuklia wakati Iran inasema mpango wake ni kwa ajili ya matumizi ya amani.