1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya: Kanda ya Euro iko salama

24 Machi 2023

Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Christine Lagarde amewaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya kwamba sekta ya kibenki ya kanda inayotumia sarafu ya Euro ina uwezo wa kile alichokiita kuhimili.

https://p.dw.com/p/4PDim
Deutschland Christine Lagarde bei der EZB-Ratssitzung mit Zinsentscheidung
Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Hayo yameelezwa na afisa mmoja aliyemnukuu Lagarde baada ya hisa za benki za Ulaya kuporomoka. Lagarde amenukuliwa katika mkutano wa kilele wa  viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini, Brussels, nchini Ubelgiji, akisema sekta ya kibenki ya kanda ya sarafu ya Euro inaweza kuhimili kwa sababu ina  mtaji imara  na uwezo thabiti wa kubadilisha mali zake katika fedha bila ya kuathiri bei kwenye masoko yake ya fedha.

Kwa upande mwingine baada ya hisa za benki ya Ujerumani, Deutsche Bank kuporomoka, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz  amesema sekta hiyo ya Umoja wa Ulaya iko imara.

''Benki ya Ujerumani Deutsche Bank, imefanya mageuzi ya kisasa katika namna inavyofanya kazi. Ni benki inayoingiza faida kubwa.Hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.''

Soma pia:  Christine Lagarde: Uchumi wa kanda ya Ulaya utakuwa bora zaidi mwaka huu

Kadhalika waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte baada ya mkutano huo wa Brussels amesema hakuna uwezekano wa kanda ya Euro kuingia kwenye mgogoro mpya wa sekta hiyo ya kibenki.