1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Waislamu na chama cha AfD wavunjika Ujerumani

24 Mei 2016

Mkutano uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kati ya Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD na kundi la Kiislamu umemalizika kwa mabishano makali Jumatatu (23.05.2016) na kuvunjika nusu saa tu baada ya kuanza.

https://p.dw.com/p/1ItVr
Picha: Reuters/A. Schmidt

Mkutano uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kati ya Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD na kiongozi wa kundi la Kiislamu umemalizika kwa mabishano makali Jumatatu (23.05.2016) na kuvunjika nusu saa tu baada ya kuanza, huku kiongozi wa kundi hilo la Kiislamu akisema chama hicho cha sera kali za mrengo wa kulia ndicho kilichoamuwa kuuvunja mkutano huo.

Mwenyekiti mwenza wa chama Mbadala kwa Ujerumani AfD Frauke Petry amesema hakuna kilichobakia kuzungumzia baada ya kundi hilo la Waislamu kukilinganisha chama chake na utawala wa Manazi.

Aiman Mazyek kiongozi wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) ambaye ndie aliyefanya juhudi za kufanyika kwa mkutano huo katika hoteli moja mjini Berlin amesema msimamo wa chama hicho cha AfD dhidi ya Uislamu unakiuka katiba kwa sababu unaibaguwa dini nzima ya Kiislamu.

Chama cha AfD ambacho kimeasisiwa kwa sera za kuutilia shaka Umoja wa Ulaya miaka mitatu iliopita kimekuwa kikipinga kumiminika kwa wakimbizi nchini Ujerumani ambapo mwaka jana zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja wameingia katika nchi hiyo yenye guvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya.

Chama hicho ambacho kimejishindia viti katika mabunge ya majimbo wakati wa chaguzi mbali mbali za majimbo mwezi uliopita kilitangaza kwamba "Uislamu sio sehemu ya Ujerumani " na kusema kwamba kinataka kupiga marufuku minara ya misikiti, adhana ya kuwaita watu wakati wa sala na wanawake kuvaa mabuibui ya kujifunika gubi gubi.

Dhamira ya chama cha AfD

Baada ya kuvunjika kwa mkutano huo Rais wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani Aiman Mazyek amesema chama cha Afd kimethibitisha kwamba kinakusudia kuendelea na sera yake kali ya mrengo wa kulia,kuchafuwa sifa ya Waislamu na kupalilia chuki isiokuwa na msingi.

Rais wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani Aiman Mazyek akisalimiana na Mwenyekiti Mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry mjini Berlin.
Rais wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani Aiman Mazyek akisalimiana na Mwenyekiti Mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mazyek amekaririwa akisema "Tunasema kamba katiba sio suala la mjadala kwetu.Na huo ndio msingi wa mazungumzo yetu.Nasikitika kusema kwamba chama cha AfD kimejitowa katika mkutano bila ya kutimiliza malengo yake.Na hakuna yoyote kati yao aliyekuwa tayari kuzungumzia masuala makuu katika sera yao.Miongoni mwao ni madai ya namna ya kujenga misikiti yetu,mabucha ya nyama za halali na kadhalika.“

Mazyek ambaye kundi lake linawakilisha sehemu tu ya jami ya Waislamu milioni nne nchinj Ujerumani alisema huko nyuma kwamba chama cha AfD ni chama cha kwanza cha Ujerumani tokea utawala wa Hitler ulipoidunisha na kutishia kundi zima la kidini.

Mazyek hakutenguwa kauli yake ya kukilinganisha chama hicho na utawaka wa Manazi kwa kweli alisisitiza baada ya kuvunjika kwa mkutano huo kwamba sera ya AfD inamkumbusha "zama za kiza kabisa" katika historia ya Ujerumani.

Mvutano kabla ya mkutano

Kulikuwa na mvutano mkubwa kutoka pande zote mbili kabla ya kuanza kwa mkutano huo na pengine kutokana na kujuwa mazingira ya kisiasa yanayokizunguka chama hicho cha AfD kilituma ujumbe mchanganyiko kwenye vyombo vya habari ambapo mwenyeiti mwenza wa chama hicho Jörg Meuthen amesema misikiti ni sehemu ya Ujerumani ni mahala pa kufanya ibada inabidi tu waangalie kwa makini nini kinachohubiriwa hapo.

Mwenyekiti Mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry.
Mwenyekiti Mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry.Picha: picture-alliance/dpa/F. Von Erichsen

Lakini mwenzake Frauke Petry alikuwa na kauli kali kwa kusema kwamba iwapo zaidi ya nusu ya Waislamu wanazipa umihumu zaidi sheria za Kiislamu "sharia" kuliko sheria za taifa jambo hilo litakuja kushindwa kudhibitiwa.

Mwanamama huyo amelalamika kufuatia kuvunjika kwa mkutano huo kwamba upande wa pili umekataa kuzungumzia juu ya masuala mahsusi kama vile sheria za Kiislamu na kudai chama hicho kikanushe sera yake ambayo imesema ilipitishwa kidemokrasia.

Petry amesema"Kwetu sisi mazungumzo haya daima yamekuwa ni suala la sote kuwa sawa kwani chama cha Afd ni chama cha demokrasia ambacho leo hii kina uwakilishi wa asilimia 15 ya wananchi wa Ujerumani na tunafikiri ni kiburi kwamba baraza hilo la Uislamu lenye kuwakilisha Waislamu 10.000 kati ya zaidi ya milioni nne wanaoishi nchini Ujerumani kutowa madai hayo dhidi yetu."

Sera tata

Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani lina wasi wasi na sera ya chama hicho cha Afd ya kuiapaka matope jamii nzima ya Waislamu jambo ambalo linasema ni pigo wa jamii yao na ndio lenye kuwakumbusha ukurasa mbaya wa historia yao na kukitaka chama hicho kuachana na mtizamo huo na kitendo hicho ambacho ni hatari sana kwa jamii.

Rais wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) Aiman Mazyek .
Rais wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani (ZMD) Aiman Mazyek .Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani lilikuwa likitaraji chama hicho cha AfD kitafuta sera yake kupiga maraufuku minara ya misikiti nchini Ujerumani ambayo chama hicho cha sera kali za mrengo wa kulia kinaielezea kuwa "alama ya madaraka" ambayo haiendani na katiba ya nchi.

Maudhui ya sera ya chama cha Afd yanaonekana kuzusha utata kutokana na kukana moja kwa moja kukana kauli ya Kansela Angela Merkel kwamba Uislamu ni sehemu ya Ujerumani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman