1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Asia a na Ulaya.

Mtullya, Abdu Said23 Oktoba 2008

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel awasili China kuhudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za Ulaya na Asia.

https://p.dw.com/p/FfZS
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwasili Beijing leo.Picha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewasili mjini Beijing kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya na wa bara la Asia wa jumuiya ya Asem ambapo pande mbili hizo zinatarajiwa kujadili mgogoro wa fedha  unaoikabili dunia.

 Lakini  vyama vya  upinzani nchini Ujerumani vinamtaka kansela Merkel pia ajadili suala la haki za binadamu na viongozi wa China.


Kansela  Merkel  anaefanya ziara ya siku tatu nchini  China atakuwa miongoni mwa viongozi 43 kutoka Ulaya na nchi za  jumuiya ya Asem watakaokutana kwa siku mbili katika mji mkuu wa China-Beijing  kujadili mgogoro wa fedha ambao pia unahitaji juhudi za nchi zinazoinukia kiuchumi katika kuukabili.Kansela  Merkel  amesema bila ya nchi hizo kushiriki, itakuwa vigumu kusonga mbele na shughuli  za masoko ya  fedha duniani.


Hatahivyo kiongozi  huyo wa Ujerumani anakabiliwa  na shinikizo katika  ziara yake nchini China.Mwezi   septemba mwaka jana alikutana na kiongozi wa kidini wa Tibet  anaeongoza  upinzani dhidi  ya  China.

China  inapinga mikutano  baina  ya kiongozi huyo  Da Lai Lama  na viongozi wa nchi zingine.

Wakati  huo huo vyama vya upinzani nchini Ujerumani vinamtaka kansela Merkel ajadili suala la haki za binadamu.

Kiongozi wa wabunge wa chama  cha kijani Volker Beck amesema bibi Merkel anapaswa  kuwasilisha  msimamo  wa Ujerumani kwenye mikutano yake na viongozi  wa China juu ya  suala la haki za binadamu na hasa  kuhusiana na hali ya majimbo ya  mashariki  mwa China.

Wakati  huo huo waziri mkuu wa China Wen Jiabao  amesema nchi yake inadhamiria kushirikiana kwa undani sana, na Ujerumani ili kukabili nyakati ngumu  za sasa. Waziri mkuu  Jiabao amesema hayo kwenye  mazungumzo yake  na Kansela Merkel. Amesema China inakusudia kushirikiana na Ujerumani katika juhudi  za kujenga mfumo mpya wa fedha duniani.


Hapo kesho Kansela Merkel ataungana na viongozi  wengine 42 kushiriki kwenye mkutano wa saba wa  kilele baina ya marais  na mawaziri  wakuu nchi  za Ulaya  na  za jumuiya ya Asem. Kikao hicho cha siku  mbili kitatayarisha mkutano wa viongozi kutoka nchi  20 utakaofanyika  kati kati ya mwezi Novemba kujadili  mfumo  wa fedha wa dunia. Ujerumani na  China pia zitashiriki  kwenye mkutano huo mjini Washington.