1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa ushirikiano na Afrika wakamilika

Josephat Charo5 Novemba 2007

Akiwa ameridhika rais wa Ujerumani Horst Köhler alijitokeza pamoja na rais wa Nigeria, Msumbiji, Botswana, Madagascar na Benin, baada ya kumalizika mkutano wa tatu wa mradi wa ushirikiano na Afrika.

https://p.dw.com/p/C7fK
Horst Köhler
Horst KöhlerPicha: AP

Wajumbe wa mkutano kuhusu ushirikiano na Afrika walisisitiza umuhimu wa utandawazi katika kuwawezesha watu lakini rais wa Ujerumani, Horst Köhler amesisitiza kwamba kila rais aliyehudhuria mkutano huo anatakiwa kwanza arekebishe mambo katika nchi yake. Ushauri huo ulitolewa pia kwa Umoja wa Ulaya ambao unazishinikiza nchi za kiafrika zisaini mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ambayo inazitaka pande hizo mbili ziyafungue masoko yao.

Pia Umoja wa Ulaya umetakiwa utimize lengo la maingiliano ya kiuchumi na bara la Afrika. Rais Köhler alizungumza kwa uwazi mbele ya wajumbe wa Afrika kabla mkutano kumalizika na kugusia umuhimu wa mikataba mizuri zaidi kwa bara la Afrika.

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya haitaki kubadili msimamo wake kuhusu makubaliano hayo. Mbali na ukweli kwamba halmashauri hiyo inalishinikiza bara la Afrika na mikataba mbalimbali rais Köhler hakuweza kujizuia kuchukua msimamo tofauti.

´Ninapoona kwamba barani Afrika sera ya Umoja wa Ulaya ya umoja na kuwajumuisha wageni inaheshimiwa, na muundo wa Umoja wa Afrika umechukuliwa kutoka kwa Umoja wa Ulaya, basi pia naweza kusema kuwa ni sawa na ni haki kwa Umoja wa Ulaya usijaribu kuugawa muungano wa Afrika kupitia mikataba mbalimbali.´

Viongozi wote wa Afrika walitoa mwito kuwepo utawala bora wa kidemokrasia. Rais wa Nigeria, Umaru Yar´ Adua alipoulizwa ikiwa rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ahudhurie mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika mjini Lisbon nchini Ureno, alisema

´Kinachoendelea nchini Zimbabwe hakihusiani na sheria za katiba. Mada kwenye mkutano wa kilele kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya kama ushirikiano na Afrika, bila shaka ni muhimu mno kuliko kuuhatarisha mkutano kwa matatizo yanayoendelea katika nchi moja. Ipo haja ya kutofautisha. Wasiwasi wa kiongozi wa serikali ni kuwa Zimbabwe kama nchi inatakiwa kuwa na haki ya kushiriki kwenye mkutano huo kwa kuwa ni sehemu ya Afrika.´

Katika mahojiano yake na mkurugenzi wa idhaa za Afrika na Mashariki ya Kati, wa Redio Deutsche Welle, Ute Schaeffer, mwenyekiti wa kamati ya African Peer Review Mechanism, bwana Bethuel Kiplagat kutoka Kenya alisema mradi wa ushirikiano na Afrika ni mzuri.

´Ama kweli mpango huo ni mzuri sana. Unawaleta pamoja viongozi wa Afrika na kwa sisi kukaa meza moja lazima niseme ni jukwaa la kipekee. Huu ni mdahalo kuhusu vipi tunavyoweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa dunia moja, kwa dunia bora.´

Uhamiaji haramu ulizungumziwa pia huku kwenye mkutano huo huku rais Köhler akiuleza kuwa kitendo kinachodunisha ubinadamu.