Mkutano wa usalama wa Munich Joe Biden aahidi kushirikiana zaidi na washirika wake wa Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Munich

Mkutano wa usalama wa Munich Joe Biden aahidi kushirikiana zaidi na washirika wake wa Ulaya

Rais Joe Biden ameahidi kwamba Marekani itashirikiana na washirika wake wa Ulaya katika juhudi za kukabiliana na changamoto za janga la maambukizi ya corona, ugaidi na mabadiliko ya tabia nchi.

Katika hotuba yake rais Biden amesisitiza umuhimu wa kuitetea na kuidumisha demokrasia duniani. Amewaambia viongozi wa nchi tajiri za G7 walioshiriki kwenye mkutano huo kwamba demokrasia inahujumiwa barani Ulaya na nchini Marekani. Rais Biden amesema Marekani itajizatiti katika kuuimarisha uhusiano kati yake na nchi za bara la Ulaya. 

Katika mkutano huo wa Munich wa masuala ya usalama rais huyo wa Marekani alizungumzia pia juu ya mabadiliko ya tabia nchi. Amesema suala hilo linahusu uhai wa binadamu wote na kwa ajili hiyo Biden ameirudisha Marekani kwenye mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya tabia nchi.

Juu ya janga la maambukizi ya corona, Biden amesema ushirikiano wa dunia nzima unahitajika katika juhudi za kukabiliana na janga hilo na ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua kabambe. Marekani itatenga kiasi cha dola bilioni 4.5 kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa chanjo kwa manufaa ya nchi masikini.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akishiriki kwenye mkutano wa maswala ya usalama wa mjini Munich kwa njia ya video.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akishiriki kwenye mkutano wa maswala ya usalama wa mjini Munich kwa njia ya video.

Viongozi wengine walioshiriki kwenye mkutano wa Munich kwa njia ya video ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenyekiti wa zamu, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson. Washiriki wengine walikuwa, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Kansela Angela Merkel na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pia wametangaza kutoa fedha zaidi ili kuchangia katika mpango wa chanjo, maarufu kama COVAX. Merkel amesema Ujerumani itaongeza Euro bilioni 1.5. Katika hotuba yake Kansela Merkel amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na ameeleza kuwa ushirikiano huo utapata fursa kwa mara nyingine kwa kupitia kwenye kundi la nchi tajiri za G7.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen

Kwa upande wake Halmashauri ya Umoja wa Ulaya nayo itaongeza mchango wake kutoka Euro milioni 500 hadi Euro bilioni 1.5.  Fedha hizo zitatolewa kwa nchi masikini kama msaada na mikopo. Akihutubia kwenye mkutano wa Munich, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amesisitiza umuhimu wa nchi masikini kupatiwa chanjo na kwa ajili hiyo amependekeza kwa Umaoja wa Ulaya na Marekani, mpango wa kupeleka dozi milioni 13 barani Afrika ili kwanza kuwapatia chanjo wahudumu wa afya wapatao milioni milioni 6.5.

Vyanzo:/AP/https://p.dw.com/p/3pbsA