1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Usalama mjini Munich Magazetini

Oumilkheir Hamidou
20 Februari 2017

Mkutano wa kimataifa kuhusu usalama mjini Munich, Donald Trump na vyombo vya habari na jinsi chama tawala cha Uturuki AKP kinavyojaribu kuitumia ardhi ya Ujerumani kufanya kampeni yake ya uchaguzi magazetini

https://p.dw.com/p/2XteS
Münchner Sicherheitskonferenz 2017 | Mike Pence, USA
Picha: Reuters/Bundesregierung/G. Bergmann

Tunaanzia Munich ulikomalizika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama. Gazeti la Schwäbische Zeitung linasema matarajio ya nchi za Ulaya kuelekea utawala mpya wa Marekani hayakupata jibu la kuridhisha. Gazeti linaendelea kuandika: "Nchi za Ulaya zilitaka kusikia katika mkutano huo wa kimataifa wa Usalama, nini kitasemwa na Marekani chini ya uongozi wa Donald Trump. Jibu halikuwa na uzito wowote , kwahivyo si la kutuliza mambo. Lakini hali itakua ya namna gani pindi suala hilo likiulizwa vyengine? Wamarekani, wachina na Wanyarwanda wameondoka na maarifa ya aina gani? Wamesikia makelele matupu tu! Kansela Angela Merkel alikuwa miongoni mwa wachache ambao hawakutaharuki. Ilikuwa Ulaya yenye nguvu iliyokuwa ikijadiliana na sio kuhukumiwa. Kwamba matokeo yake ni kufikiwa maridhiano ambayo si ya kuridhisha sana, hilo ni jambo la kawaida , mataifa 27 yanapokuwa na mengi ya kusema kwa wakati mmoja.

Lakini hali sasa inatisha kwa namna ambayo fikra ya Ulaya inatishia kukwama. Baadhi ya nchi za Ulaya ya mashariki zinabidi zionyeshe uvumilivu. Ulaya inakabwa na misuko suko. Watu wanabidi wajifunze kuvumilia na kuzungumza kwa sauti moja. Upande wa pili wa bahari ya Atlantik kuna uongozi usiokadirika na ambao viongozi wake hawana msimamo wa pamoja. Hali hiyo isije ikaiambukiza pia Ulaya."

Trump adharau vyombo vya habari

Rais wa Marekani Dinald Trump anaendelea kugonga vichwa vya habari, mwezi mmoja baada ya kuingia madarakani. Si habari za kuvutia lakini, linasema gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linalochambua uhusiano wa Donald Trump na Vyombo vya habari. "Donald Trump amevunja rikodi. Kwa bahati mbaya. Amegeuka kuwa rais wa kwanza wa Marekani kudharau mhimili muhimu kabisa: Uhuru wa vyombo vya habari. Anavitaja vyombo vya habari, tangu gazeti la New-York Times, au vituo vya televisheni vya NBC, ABC na CNN kuwa ni "maadui wa wananchi wa Marekani."

Trump, sio tu halijui chimbuko la muktadha huo, lakini hata kipaji cha kuona yajayo hana. Kinyume chake angewacha mtindo wake wa kuwatia kishindo waandishi habari nchini mwake, kitendo ambacho hakijawahi kuishuhudiwa tangu vilipomalizika vita vikuu vya pili vya dunia.

AKP yafanya kampeni zake katika ardhi ya Ujerumani

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kampeni ya chama tawala cha Uturuki AKP nchini Ujerumani. Gazeti la "Volksstimme" linaandika: "Ni mshangao mkubwa kuona jinsi  waziri mkuu Binali Yildirim alivyojitokeza. Ilikuwa hadhara kubwa kabisa kuwahi kuitishwa tangu vita vikuu vya pili kumalizika kumuona muimla akijipigia domo katika ardhi ya Ujerumani. Cha kutisha zaidi ni kwamba miongoni mwa jamii ya wachache ya waturuki nchini Ujerumani, wengi wanaonyesha kupinga demokrasia."

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman