1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa UN wamalizika kwa makubaliano ya kuiunga mkono UN

Isaac Gamba
2 Oktoba 2018

Viongozi wa dunia walitoa ujumbe wa pamoja juu ya haja ya kuunga mkono hoja ya ushirikiano wa pamoja. 

https://p.dw.com/p/35r9W
UN-Sicherheitsrat in New York | Donald Trump, Präsident USA
Picha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

Mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa umemalizika huku rais wa baraza kuu la Umoja huo Maria Fernanda Espinosa akisema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni dunia kuunga mkono Umoja wa Mataifa pamoja na kutilia mkazo juu ya ushirikiano wa pamoja kimataifa.

 Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Rais wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa alisema wakati wa mjadala katika mkutano huo uliochukua wiki moja mjini New York viongozi wa dunia walitoa ujumbe wa pamoja juu ya haja ya kuunga mkono hoja ya ushirikiano wa pamoja. 

Ameongeza kuwa inaleta usumbufu wakati baadhi ya nchi zinapoamua kujitoa katika wajibu wa kimataifa huku akiongeza kuwa hata hivyo dunia inalazimika kuheshimu tofauti hizo zilizopo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na rais wa Marekani Donald Trump wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na rais wa Marekani Donald Trump wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: Reuters/E. Munoz

Viongozi kadhaa walionekana kukosoa kauli ya  rais Donald Trump wa Marekani aliyoitoa wakati akilihutubia baraza hilo la Umoja wa Mataifa ambapo alizipinga nadharia za utandawazi na kusisitiza kuunga mkono misimamo ya kizalendo.

 Tangu  rais Trump ashike madaraka Marekani tayari imejitoa katika makubaliano kadhaa ya kimataifa  ikiwa ni pamoja na makubaliano ya nyukilia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani  pamoja na mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi uliosainiwa mjini Paris.

Utawala wa rais Donald Trump tayari pia umejitoa katika makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji yanayotarajiwa kuidhinishwa  mwezi Desemba nchini Morocco.

Suala la mabadiliko ya tabia ya nchi, kuzuia migogoro pamoja na suala linalohusu ushirikiano wa pamoja kimataifa  yalikuwa ni miongoni mwa masuala yaliyogusiwa na wazungumzaji wengi katika mkutano huo wakiwemo wakuu wa mataifa 77, makamu wa rais kutoka mataifa matano na viongozi 44 wa serikali.

Viongozi wa dunia walitoa ujumbe wa pamoja juu ya haja ya kuunga mkono hoja ya ushirikiano wa pamoja. 
Viongozi wa dunia walitoa ujumbe wa pamoja juu ya haja ya kuunga mkono hoja ya ushirikiano wa pamoja. Picha: Pakistan mission USA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliifungua mkutano huo leo akisema ulimwengu hivi sasa una matumaini makubwa katika ushirikiano na kuonya kuwa ushirikiano huo unaonekana kupigwa vita katika wakati ambao unahitajika zaidi.

Miongoni mwa nchi chache zilizozungumzia juu ya utaifa ni Hungary ambayo ilijenga waya wa Sen'genge ili kuzuia wahamiaji .

 Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Peter Szijjarto alisema uhamiaji ni changamoto na kuwa wimbi la wahamiaji linasababisha changamoto kubwa kiusalama na pia linaleta ugaidi katika maeneo ambayo hayajawahi kuwa na historia ya matukio ya kigaidi.

Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman