Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi waanza leo. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 20.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi waanza leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo anafungua mkutano kuhusu ubaguzi, ambao tayari umeingiwa na dosari baada ya nchi kadhaa za magharibi kujitoa na wasiwasi kwamba Rais wa Iran atatoa matamshi mengine dhidi ya Israel.

default

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad ambaye kuhudhuria kwake mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi mjini Geneva, kumesababisha baadhi ya nchi za magharibi kususia mkutano huo kwa hofu ya kiongozi huyo kutoa matamshi ya kuishambulia Israel.

Rais Mahmoud Ahmadnejad wa Iran ambaye aliwahi kusema Israel iondolewe katika ramani na kuelezea mauaji ya Wayahudi kuwa ni uongo aliwasili jana jioni mjini Geneva akiwa ni miongoni mwa viongozi wachache wanaohudhuria mkutano huo.

Rais huyo wa Iran, ambaye anagombea tena kuchaguliwa katika nafasi yake hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini humo mwezi June, alinukuliwa na Radio ya Taifa ya nchi hiyo akisema kwamba itikadi za kiyahudi na mfumo wa utawala ni mwenendo wa ubaguzi.

Maoni kama hayo yalitolewa na nchi za Kiarabu na za Kiafrika miaka minane iliyopita na kuchochea Marekani na Israel kutoka nje wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Ubaguzi uliofanyika Durban Afrika kusini na kwamba mkutano wa siku tano wa Geneva unaofanyika wiki hii unaenda katika kile Israel imekiita tukio la kipuuzi hata kabla ya kuanza kwake.

Baraza la Wayahudi barani Ulaya lenye makao yake mjini Paris, pia limepinga kushiriki kwa kiongozi wa Iran katika mkutano huo.

Uamuzi wa serikali ya Marekani ulitolewa siku ya Jumamosi kuungana na Canada na Israel kujitoa katika mkutano huo na kufuatiwa na Australia, Ujerumani, Italia, Uholanzi na New Zeland.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Australia Stephen Smith amesema wanasikitika, hawana uhakika kwamba mkutano huo hautatumiwa tena kama ulingo wa kutoa mitazamo ya kuchukiza ikiwemo misimamo dhidi ya Israel.

Jana nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya nazo ziligawika iwapo kuifuata Marekani katika kususia mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi, huku Ujerumani ikiwa nchi ya mwisho kutangaza uamuzi huo wa kutoshiriki mkutano huo na Ubelgiji ikitoa wito kwa nchi hizo kushiriki mkutano huo.

Uingereza na Ufaransa zimesema zitashiriki mkutano huo.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa amesema balozi wa nchi hiyo mjini Geneva, atahudhuria mkutano huo, lakini atatoka nje haraka iwapo mkutano huo utageuka kuwa ulingo wa kuikosoa Israel.


Mkutano huo wa Geneva unalenga kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya Ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na na hali isiyovumilika tangu kufanyika kwea mkutano wea dunia dhidi ya ubaguzi mwaka 2001, mjini Durban Afrika kusini, kama anavyoelezea zaidiKamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu Navi Pillay.


Wakati huohuo, wakati shambulio ,lililofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza hivi karibuni likiendelea kuumiza mioyo, asasi za kiraia zimekusanyika mjini Geneva kuzungumzia uhalifu huo wa kijeshi wa Israel na ubaguzi.

Mwandishi: Halima Nyanza/AFP/IPS

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
 • Tarehe 20.04.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/AFP/IPS
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HaQC
 • Tarehe 20.04.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/AFP/IPS
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HaQC
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com