1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa uhai-anuai waendelea huko Nagoya, Japan

Kabogo Grace Patricia20 Oktoba 2010

Mkutano huo una lengo la kuzuia kutoweka kwa viumbe hai, mazingira na mimea.

https://p.dw.com/p/PjRq
Wajumbe wakiwa katika mkutano wa uhai-anuai huko Nagoya, Japan.Picha: picture alliance/dpa

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa serikali na biashara duniani kote zinahitaji kutambua thamani kubwa ya kiuchumi ya kuhifadhi viumbe hai, mazingira na mimea ikiwa ni pamoja na kuyazingatia masuala hayo pindi wanapofanya maamuzi yao. Ripoti hiyo imetolewa hii leo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhai-anuai unaofanyika Nagoya, Japan wa kuzuia kutoweka kwa viumbe hai na mazingira asilia.

Ripoti hiyo ya Uchumi, Mazingira na Uhai-Anuai-TEEB, inajaribu kuonyesha jinsi athari za kiuchumi zinavyoshindwa kuzuia suala la kupotea kwa viumbe hai mbalimbali na mazingira kutokana na uchafuzi au uharibifu wa mazingira unaopindukia. Katika ripoti hiyo, Mradi wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa-UNEP, unatilia mkazo zaidi umuhimu wa kubadilika kwa shughuli zinazofanywa viwandani, migodini na uzalishaji wa nishati ya umeme.

Pavan Sukhdev ambaye ameongoza utafiti uliofanywa kwa muda wa miaka mwili na kuungwa mkono na UNEP anasema kuwa muda wa kudharau uhai-anuai na kuendelea kufikiria kuhusu utajiri wa kawaida pamoja na maendeleo, umepitwa na wakati. Ripoti hiyo ya TEEB iliyowajumuisha mamia ya wataalamu kutoka duniani kote, ina lengo la kuongeza uelewa wa kimataifa katika gharama kubwa ya kifedha ya kutokuchukua na kukuza matumizi endelevu ya mazingira.

Ripoti hiyo pia imefafanua kuwa misitu na mazingira mengine inachangia katika maisha ya kila siku ya mwanadamu katika maeneo ya mijini na pia yana umuhimu katika kusaidia kuwapa wanadamu afya, mali, chakula, maji, mafuta na mambo mengine muhimu katika maisha ya binadamu ikiwemo kupunguza umasikini. Watu wengi wanashindwa kuelewa ni kwa kiasi gani mwanadamu anategemea mazingira katika kuendesha maisha yake.

Ripoti hiyo pia imesema suala la kupambana na uvuvi uliokithiri ambao kwa sasa ungetakiwa kutiwa moyo kutokana na kutolewa ruzuku kwa viwanda vya samaki pamoja na kuepukana na kanuni na utekelezaji hafifu, lingeweza kuruhusu hifadhi ya samaki baharini duniani kote kuongezeka na kufikia kuwa na thamani ya Dola bilioni 50 zaidi kwa mwaka. Msemaji wa UNEP Nick Nuttall anasema kuwa nchi kama India na Brazil tayari zimeanza kuchukua hatua za kutumia njia za TEEB.

Waziri wa Mazingira na Misitu wa India, Jairam Ramesh amesema kuwa TEEB ina lengo la kutoa motisha kwa nchi kuhakikisha maamuzi siyo tu kwa kuzingatia mafanikio ya muda mfupi, bali pia kujenga misingi ya umoja na maendeleo endelevu. UNEP imeeleza kuwa Halmshauri ya Umoja wa Ulaya pamoja na Ujerumani ziliona faida ya TEEB katika mkutano wa mawaziri wa mazingira wa kundi la mataifa tajiri duniani-G8, uliofanyika Postdam mwaka 2007. Ripoti hiyo ya TEEB ilifadhiliwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Uingereza, Uholanzi, Norway, Ubelgiji, Sweden na Japan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/APE)

Mhariri:M.Abdul-Rahman