Mkutano wa Syria wataka kuimarisha amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa Syria wataka kuimarisha amani

Marais wa Uturuki, Iran na Urusi wamesema wanania ya kuhakikisha "utulivu nchini Syria " na kuwalinda raia katika  maeneo yaliyotengwa kuwa na utulivu, kwa mujibu wa  mkutano wao uliojadili amani  ya Syria.

Taarifa  hiyo  ya  pamoja  ya  viongozi  hao  Recep Tayyip Erdogan , Vladimir Putin  na  Hassan Rouhani   iliwekwa  katika  tovuti  ya  rais wa  Iran  baada  ya  mkutano  wao wa  kilele  uliofanyika  mjini Ankara  nchini  Uturuki.

Viongozi  hao  walifanya  mkutano   na  kila  mmoja  wao  kwa nyakati  tofauti  kabla  ya  kuanza  kwa  mkutano  wa  pande  tatu, ambao  uliiweka  kando  Marekani , nchi  nyingine  ya  kigeni  yenye majeshi  yake  nchini  Syria.

Russland | Präsidenten Erdogan, Putin und Rouhani (picture-alliance/AP Images/K. Ozer)

Viongozi wa Urusi, Uturuki na Iran, Hassan Rouhani, Vladimir Putin (katikati9 na tayyip Erdogan kabla ya mkutano kuhusu Syria

Mataifa  hayo  matatu  yanasukuma kile  kinachojulikana  kama mchakato  wa  Astana , ambao  una  lengo  la  kuweka  "maeneo ya kutuliza  vita"  nchini Syria. Licha  ya  hayo, mataifa  yote  matatu yanabakia  kuwa  wahusika  wakubwa  katika  vita  vya  wenyewe kwa  wenyewe  nchini  humo.

Rais  wa  Iran  Hassan Rouhani  ameilaumu  Marekani  kwa  kuliunga mkono  kundi  la  wanamgambo  linalojiita  Dola  la  Kiislamu  nchini Syria  na kutoa  wito  kwa  nchi  zote  kuheshimu uhuru wa  mshirika wake  mkubwa  katika  mataifa  ya  kiarabu  katika  mashariki  ya kati , imesema  televisheni  ya  Iran.

Baadhi  ya  nchi  ikiwa  ni  pamoja  na  Marekani , wanaunga  mkono makundi  ya  kigaidi  kama  Dola  la  Kiislamu  nchini  Syria, ambalo linalinda  maslahi  ya  nchi  hizo, Iran ikiamini mzozo  wa  Syria hauna suluhisho  la  kijeshi na  kuulinda  uhuru  wa  Syria kuwa  ni jambo  muhimu kwa  Tehran," Rouhani  aliwaambia  waandishi habari  mjini  Ankara.

Türkei Erdogan mit Ruhani in Ankara (Reuters/Presidential Palace/K. Ozer)

Rais wa Iran Hassan Rouhani (kushoto) na Recep Erdogan (kulia)

Mipaka ya Syria iheshimiwe

Nae  rais  wa  Uturuki Tayyip Erdogan  amesema  kwamba  uhuru wa  mipaka  ya  Syria  unategemea kujiweka  mbali  na  makundi yote  ya  kigaidi , akimaanisha  Marekani  kuliunga  mkono  kundi  la wanamgambo  wa  Kikurdi  nchini  Syria ambalo  Uturuki  inaliona kuwa  ni  adui.

Erdogan  amesema  kwamba  matumaini  ya  kupata  mafanikio nchini  Syria  yanaongezeka. Na kusema  kwamba  Uturuki  na  Urusi zitafanyakazi kwa pamoja  kujenga hospitali  katika  eneo  la  Tel Abyad  nchini  Syria  kuwatibu wale  wanaokimbia  kutoka  Ghouta mashariki. Amesema  majeshi  ya  Uturuki  na  Urusi  yatashirikiana kujenga  hospitali  hiyo.

Kwa upande  wake  rais Donald Trump  ambaye  nchi  yake hakualikwa  kuhudhuria  mkutano wa  nchi  tatu  zinazohusika  katika mzozo  wa  Syria  amekubali  katika  kikao  cha  baraza  la  usalama la  taifa  kuendelea  kuviweka  vikosi  vya  majeshi  ya  nchi  hiyo nchini Syria kwa  muda  zaidi  lakini  anataka  viondoke haraka iwezekanavyo, amesema  afisa  mwandamizi wa  utawala  huo leo.

USA | Trump kündigt militärischen Rückzug aus Syrien an (Getty Images/J. Swensen)

Rais Donald Trump wa Marekani

Wakati  huo  huo Umoja  wa  Mataifa  umesema  leo kwamba umepeleka  ujumbe  wake  wa  kwanza  wa  kiutu  mjini  Raqa  tangu mji  huo  wa  Syria  kukombolewa  kutoka  udhibiti  wa  kundi  la  Dola la  Kiislamu, ukionya kwamba  raia  wanaorejea  wanakabiliwa  na mzigo  mkubwa. Mji  huo  ambao  kundi  la  IS  liliutangaza  kuwa sehemu  ya utawala  wake  wa  kikhalifa mwaka  2014, umetapakaa mabomu  ambayo  hayaja  ripuka, mkuu wa  ujumbe  wa  kutoa misaada  ya  kiutu  wa  Umoja  wa  mataifa  nchini  Syria , Jan Egeland  aliwaambia  waandishi  habari mjini  Geneva leo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre/ afpe / dpae

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com