Mkutano wa nchi za G8 kuanza kesho Japan | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano wa nchi za G8 kuanza kesho Japan

Japan na Marekani zataka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya bei za mafuta na chakula

Hoteli ya Windsor mjini Toyako kisiwani Hokkaido kutakakofanyika mkutano wa G8

Hoteli ya Windsor mjini Toyako kisiwani Hokkaido kutakakofanyika mkutano wa G8

Marekani na Japan leo zimetaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya kupanda kwa kasi bei za mafuta na chakula ambazo huenda zikaubadili mkondo wa uchumi wa dunia.

Haya yamejitokeza baada ya rais wa Marekani Geroge W Bush kukutana leo na waziri mkuu wa Japan Yasuo Fukuda mjini Toyako, siku moja kabla kuanza kwa mkutano wa nchi tajiri kiviwanda duniani, G8. Mkutano huo unatarajiwa kuanza hapo kesho mjini Toyako kisiwani Hokkaido nchini Japan.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini humo rais Bush amezungumzia bara la Afrika akisema wakati umefika kwa nchi za G8 kulisaidia bara la Afrika.

``Wasiwasi wangu kuhusu Afrika unaanza kwa kujua kwamba watu wengi mno wanakufa kutokana na ukimwi.Na ndio maana bunge la Marekani na liliungana na serikali kusaidia juhudi za kuwasaidia watu kupata dawa za kupunguza makali ya ukimwi nakuwasaidia mayatima. Kwa sasa bara la Afrika linakabiliw ana matatizo mengi na huu ndio wakati nchi zilizoendelea zichukue hatua kuyatatua.´´

Rais wa Urusi Dmitry Medvedev amewasili leo nchini Japan kuhudhuria mkutano huo wa mataifa ya G8. Kwa mara ya kwanza tangu kuapishwa kuwa rais wa Urusi, Medvedev atakutana na rais Bush na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown huku uhusiano kati ya Uingereza na Urusi ukiwa katika hali ya kulegalega.

Mzozo wa Zimbabwe

Japan imesema leo kwamba viongozi wa nchi za G8 watajadili kuichukulia hatua kali Zimbabwe kufuatia uchaguzi uliokolewa na jumuiya ya kimataifa.

Waziri mkuu wa Canada, Stephen Harper, amelizusha swala la Zimbabwe wakati wa mkutano wake na waziri mkuu wa Japan Yasuo Fukuda. Waziri mkuu Fukuda amesema wana wasiwasi na hali nchini Zimbabwe na kutaka hatua za haraka zichukuliwe.

Marekani imesema mkutano wa kilele wa G8 utamlaani vikali rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika taarifa itakayotolewa mwishoni mwa mkutano huo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema viongozi watakaohudhuria mkutano huo wa kilele wa G8 watajadiliana na njia za kuiongezea vikwazo Zimbabwe na kutoa mwito nchi za Afrika ziviunge mkono vikwazo hivyo.

 • Tarehe 06.07.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EXJK
 • Tarehe 06.07.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EXJK
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com