1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO unafungua pazia mjini Washington

10 Julai 2024

Viongozi wa NATO wanakutana leo mjini Washington kwa mkutano wa kilele wakilenga kutanua uungaji wao mkono kwa Ukraine na kuimarisha mshikamano chini ya kiwingu cha mashaka yanayouandama ulimwengu wa magharibi.

https://p.dw.com/p/4i6Pp
Mkutano wa kilele wa NATO wa Marekani mjini Washington | Rais Biden
Rais Joe Biden akitoa hotuba kwenye maadhimisho ya miaka 75 ya NATO katika Ukumbi wa Andrew W. Mellon, Julai 9, 2024, mjini Washington.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo unaokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 75 tangu kuundwa kwa mfungamano huo wa kijeshi, umetanguliwa na dhifa ya kufana iliyofanyika usiku wa kuamkia leo mjini Washington. Mwenyeji wa mkutano huo Rais Joe Biden anadhamiria kuhimiza mshikamano thabiti miongoni mwa wanachama 32 wa NATO pamoja na kuwahakikishia wapiga kura wa Marekani kwamba yungali anao uwezo wa kuhudumu muhula wa pili madarakani. Mkutano huo wa siku tatu utajadili pamoja na mambo mengine msaada wa nyongeza wa kijeshi kwa Ukraine na washirika wengine wa NATO. Rais Volodomyr Zelensky na viongozi wa mataifa ya Japan, Korea Kusini, Australia na New Zealand ni miongoni mwa wale walioalikwa kuhudhuria mkutano huo.