Mkutano wa Maji wa Kimataifa watafuta suluhisho kwa tatizo la maji duniani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 16.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano wa Maji wa Kimataifa watafuta suluhisho kwa tatizo la maji duniani

Wanasiasa,wakurugenzi wa makampuni,wahandisi na wanaharakati wa mazingira wamekusanyika mjini Istanbul Uturuki kuhudhuria mkutano wa juma moja kwa lengo la kupambana na tatizo la maji duniani linalozidi kuwakubwa

Mwanamke akichota maji nchini Peru

Mwanamke akichota maji nchini PeruKiasi ya wajumbe 20,000 wanatazamiwa kushiriki katika Mkutano wa Tano wa Maji wa Kimataifa mjini Istanbul ulioitishwa na Baraza la Maji Duniani. Wajumbe hao watakabiliana na ajenda iliyojaa masuala tete - kwa mfano, maji safi na huduma za usafi,uchafuzi wa mito, mivutano inayohusika na udhibiti wa maji na bila shaka athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.


Ripoti ya kurasa 348 iliyotolewa na mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa kabla ya mkutano unaoanza leo hii,imeonya kuwa tatizo la maji duniani linaweza kusababisha machafuko,mivutano na migogoro kati ya mataifa.

Mkuu wa Baraza la Maji Duniani Loic Fauchon amesema,ukweli ni kuwa hali ya mambo imebadilika.Enzi ya kupata maji kwa urahisi imepita.Sasa wakati umewadia kuanzisha sera za kurekebisha mahitaji yetu ya maji. Miaka hii 50 iliyopita,sera za maji kote duniani zilishughulikia njia za kupata maji zaidi. Katika baadhi ya nchi matumizi ya maji yamefikia viwango vya kuaibisha.Amesema,sote hapa duniani tunapaswa kutia maanani uhusiano wa binadamu na maji na kujaribu kupunguza matumizi yetu ya maji.Matumizi mengine ya uharibifu ni umwagiliaji maji unaopindukia kiasi ambapo mazao yanayohitaji maji mengi hupandwa katika maeneo yenye ukame wa asilia.


Kwa mfano katika enzi ya Soviet Union,miradi ya kupanda pamba katika jangwa la Asia ya Kati imesababisha maji kupunguka katika ziwa la Aral ambalo hapo zamani lilikuwa ziwa kubwa la nne duniani. Hata mifumo ya umwagiliaji maji inayotumiwa katika eneo la bonde huko California Marekani na kwenye mto Murray-Darling nchini Australia mara kwa mara hutajwa kwa uharibifu wa aina hiyo.


Lengo kuu la mkutano wa Istanbul ni kutafuta njia za kuepusha "vita vya kugombea maji" kwa kuhimiza makubaliano kati ya mataifa ili yaweze kutumia pamoja mito na maziwa yanayovuka mipaka ya nchi jirani. Kwa mujibu wa duru zilizo karibu na mkutano huo,Uturuki,Iraq na Syria zinatazamiwa kutangaza makubaliano ya kugawana maji yanayotoka kwenye mito Tigris na Euphrates.

Mkutano wa Maji utafikia kilele chake siku tatu za mwisho,pale utakapofanywa mkutano wa mawaziri kutoka nchi 107. Na tarehe 22 Machi, mkutano huo utakamilishwa kwa kutolewa hati ya mapendekezo yasiyo shurutisha.


Mwandishi: Prema Martin /AFPE

Mhariri: Miraji Othman • Tarehe 16.03.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HCuw
 • Tarehe 16.03.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HCuw
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com