1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa mjini Bonn

10 Agosti 2009

Kuanzia leo Jumatatu,wajumbe wa serikali za nchi wanachama 192 waliotia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa wanakutana mjini Bonn kwa majadiliano yasio rasmi hadi Agosti 14.

https://p.dw.com/p/J6sv
Umweltminister Sigmar Gabriel vor Rügen auf dem 30-Meter-Zweimaster „Gotland“ Copyright: DW
Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel.Picha: DW

Wajumbe hao watatayarisha mswada wa mkataba utakaowasilishwa katika mkutano wa kilele utakaofanywa Copenhagen katika mwezi wa Desemba. Katika mikutano ya Bonn wajumbe watakuwa na kazi kubwa mpaka utakapopatikana mkataba unaohusika na hatima yetu. Kwani mkataba huo unahusika na mabadiliko ya hali ya hewa-suala lenye umuhimu mkubwa mno kwa mustakabali wa binadamu hapa duniani.

Katika mkutano wa mwisho wa kundi la nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8 uliofanywa katika mji wa L´Aquila nchini Italia, nchi zote nane ikiwemo pia Marekani, zilikubaliana kuwa na lengo moja-yaani hadi mwaka 2050 ongezeko la joto lisipindukie nyuzi joto 2 za Celsius. Lakini watafiti wa hali ya hewa na mashirika yanayohusika na ulinzi wa mazingira kama vile Greenpeace, wanaamini kuwa hata ongezeko la sentigredi mbili ni nyingi mno. Martin Kaiser anaeongoza tume ya Greenpeace katika mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn anasema:

"Ongezeka kama hilo litamaanisha kuwa misitu ya Amazon haitokuwepo tena duniani kama misitu yenye mvua kubwa; usawa wa bahari utakwenda juu kwa mita moja zaidi: na mashamba mengi yatakauka kwa kiasi ambacho wala hayatofaa kulimwa tena."

Kwa jumla,kulipangwa kuwepo duru tano za majadiliano kabla ya mkutano wa Copenhagen nchini Denmark hapo mwezi wa Desemba ambako mataifa 192 yanatazamiwa kuidhinisha mkataba wa karne, kuhusu ulinzi wa mazingira. Mikutano miwili ya kwanza ilifanywa mjini Bonn. Mkutano wa juma hili ni mkutano usio rasmi na utafuatwa na mikutano miwili mingine - katika mji wa Bangkok kati ya Septemba na Oktoba na mjini Barcelona mwanzoni mwa mwezi wa Novemba. Mkutano utakaofanwa Desemba mjini Kopenhagen unatazamiwa kuidhinisha mkataba utakaochukua nafasi ya Mkataba wa Kyoto ambao unamalizika mwaka 2012.

Mkutano wa Bonn uliopita, ulikusanya hati ya kurasa 300 zenye mapendekezo ya washirika 192. Kazi kubwa ya mkutano wa juma hili ni kuzipunguza kurasa hizo kufikia 50 hadi 100 na kuiwasilisha hati hiyo Copenhagen ambako baada ya kujadiliwa na viongozi wa nchi na serikali, inatarajiwa kutiwa saini.

Mpaka sasa, tatizo kuu ni nani anaepaswa kupunguza utoaji wa gesi chafu, zinazoathiri hali ya hewa; ipungzwe kwa kiwango gani na kwa muda gani. Na je,nani atakaetoa msaada wa fedha kwa nchi zinazoendelea, ikiwa nchi hizo zitatataka kufanya mabadiliko ya muda mrefu, ili ziwe na uchumi usiochafua mazingira. Kwa hivyo, wajumbe katika mikutano ya juma hili mjini Bonn watatayarisha mswada wa mkataba, baada ya kupitia mapendekezo mbali mbali yaliyowasilishwa.

Mwandishi: H.Jeppesen / ZPR / P.Martin

Mhariri:Abdul-Rahman