1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mkutano wa kujipigia debe"

Maja Dreyer13 Novemba 2007

Ghasia zilizoanzishwa na washabiki wa soka nchini Italy ambapo mmojawao aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, vilevile mkutano wa mabaraza ya mawaziri wa Ufaransa na Ujerumani hapo jana – hizo ndizo baadhi ya mada zilizozingatiwa na wahariri wa magazeti leo hii.

https://p.dw.com/p/CHRf
Picha ya uwongo?
Picha ya uwongo?Picha: AP

Kwanza ni gazeti la “Braunschweiger” ambalo linachunguza uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa. Limeandika:

“Tumeshawahi kusikia uwongo mzuri zaidi kwenye jukwaa la kidiplomasia. Maneno haya mazuri lakini yaliyosikika jana hayawezi kuficha hali halisi ya uhusiano ambao si mzuri sana. Kuna migogoro, ukosefu wa maelewano na tofauti za maoni. Tangu rais mpya Nicolas Sarkozy alipohamia kwenye ikulu ya Ufaransa ni kama vile iko hali ya hatari kati ya Ujerumani na Ufaransa. Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ambao zamani ulikuwa kama injini ya Umoja wa Ulaya bado haujaanza kufanya kazi tena.”

Mhariri wa gazeti la “Rheinische Post” anaona kwamba mkutano huu wa viongozi na mawaziri umeandaliwa vizuri ukiwa na lengo moja hasa. Ameandika:

“Baada ya migogoro kati ya Kansela wa Ujerumani na rais wa Ufaransa, mkutano huu wa Berlin ulilenga kuonyesha picha ya maelewano. Basi, lengo hili limefikiwa. Licha ya hayo lakini hakuna mengi yaliyotokea. Mkutano huu wa kilele ulilenga tu kujipigia debe. Afadhali mawaziri hao wakutane tu kufanya kazi.”

Suala la pili: Baada ya ghasia na kifo cha shabiki mmoja wa soka huko Italy, polisi na majaji sasa wanataka kuchukua hatua kali dhidi ya mashambulizi. Wahariri wanachambua hali ya mchezo wa kandanda nchini Italy. Katika gazeti la “Allgemeine Zeitung” la mjini Mainz tunasoma hivi:

“Mchezo wa soka katika nchi ambayo ni bingwa wa dunia umeporomoka. Ni mchangayiko wa makosa yaliyosababisha ghasia nchini Italy. Kupigwa risasi kwa shabiki mmoja na polisi kulikuwa kama bahati mbaya. Uamuzi wa kuchukua hatua kali baada ya michafuko ni suluhisho lisilofaa. Wala siasa wala wakuu wa vilabu vya soka wamelifahamu jukumu lao ni lipi.”

Na mhariri wa “Frankfurter Rundschau” amenandika:
“Nchi hiyo bingwa wa dunia wa soka ina viwanja vibaya zaidi vya mataifa makuu. Vilevile kuna rushwa nyingi katika ligi yao. Italy haijapinga wachezaji wao maarufu kutaja itikadi zao za kibaguzi wala haijachukua hatua dhidi ya mashabiki wa mrengo mkali wa kulia kuonyesha alama zao uwanjani. Kwa hivyo, tatizo hili limelelewa nchini Italy. Ujerumani inapaswa kuwa na uangalifu kutoelekea katika hali hiyo hiyo, kwani katika ligi kadhaa hususan Mashariki mwa Ujerumani tayari kuna makundi makubwa wa Manazi miongoni mwa Mashabiki.”

Na hatimaye ni gazeti la “Die Tagespost” ambalo linahitimisha hivi matokeo nchini Italy:

“Ikiwa wanasiasa husika watashindwa kuupa kipaumbele mchezo wenyewe na kuwafahamisha raia, basi itabidi wachezaji wafunge goli bila ya kushangiliwa na watangazaji.”