1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa wa UKIMWI

P.Martin4 Agosti 2008

Mkutano wa kimataifa wa UKIMWI umefunguliwa Mexico City kwa wito wa kuimarisha juhudi za kupiga vita ugonjwa uliosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 25 tangu ugonjwa huo kugunduliwa mara ya kwanza mwaka 1981.

https://p.dw.com/p/EqOl

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon siku ya Jumapili alipofungua mkutano huo wa siku sita,alitoa wito kwa mataifa fadhili kutimiza ahadi zilizotolewa na Umoja wa Mataifa na kundi la madola manane tajiri duniani G-8,kuwa wagonjwa wote walioambukizwa virusi vya UKIMWI waweze kupatiwa dawa za kurefusha maisha ifikapo mwaka 2010,.Amesema,bado tunakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha wakati vita dhidi ya UKIMWI vikikaribia kutimiza miongo mitatu.Akaongezea:

"Jitahada za kupambana na HIV na UKIMWI zinahitaji fedha kwa muda mrefu unaoselelea.Kwani kila watu zaidi wakipata matibabu na kuishi muda mrefu zaidi,basi bajeti pia zitapaswa kuongezwa kwa wingi."

Hivi sasa watu milioni 33 wanaishi na virusi vya UKIMWI.Asilimia 90 ya wale walioambukizwa wanaishi katika nchi masikini.Ingawa tangu miaka miwili iliyopita msaada kwa watu hao uliimarishwa,hivi sasa watu milioni tatu tu ndio hapata dawa zinazorefusha maisha yaani chini ya theluthi moja ya wale wanaohitaji matibabu.

Vita dhidi ya UKIMWI vitakuwa virefu ameonya,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa-WHO,Bibi Margaret Chan.Na UNAIDS,Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na miradi ya kupambana na UKIMWI limesmea kuwa mwaka jana,kama dola bilioni kumi zilitumiwa kupiga vita UKIMWI katika nchi masikini.Hilo ni ongezeko kubwa kulinganishwa na fedha zilizotumiwa mwanzo wa mwongo huu.Lakini hata hivyo bado miradi ya kupambana na ukimwi imepungukiwa na kama dola bilioni nane.

Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huo wa kimataifa kuhusu UKIMWI kufanywa katika Latin Amerika,ambako watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo,hutazamwa kama watu waliopata aibu.Safari hii mkutano huo wa siku sita unahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 22,000 ikiwa ni pamoja na wanasayansi,wanasiasa na wafanyakazi wanaoshughulikia miradi ya kupiga vita UKIMWI.

Leo Jumatatu,rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton anahotubia mkutano huo na anatazamiwa kutoa wito wa kuwapatia dawa za kurefusha maisha,wagonjwa wote walioambukizwa virusi vya UKIMWI katika nchi masikini.