1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kilele wa Vijana Msituni Bavaria

S.Sand/P.Martin26 Mei 2008

Vijana 50 kutoka nchi 18 walishiriki katika mkutano wa kimataifa wa vijana,kuhusu uhai anuai.Vijana hao walikutana kambini Falkenstein kuanzia Mei 16 hadi 24 kwenye mbuga ya taifa katika jimbo la Bavaria.

https://p.dw.com/p/E6Rh

Mkutano huo ulifanywa sambamba na ule mkutano wa 9 wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn juu ya njia za kulinda na kuhifadhi mimea na viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka yaani uhai anuai.Vijana hao walipata nafasi ya kutayarisha mradi uliojumuisha hisia zao kuhusu mada hiyo pamoja na tamaduni zao mbali mbali.Mapendekezo yao yamewasilishwa mkutanoni Bonn na yanashughulikiwa hadi 30 Mei.Huko kambini katika Mbuga ya Taifa,Lukas Laux anaesimamia miradi ya elimu amesema:

"Tumefikiria kuwa na mkutano wa kimataifa kambini kwa sababu katika msitu huu tuna vibanda tofauti kutoka nchi mbali mbali.Vile vile tunashirikiana na miradi ya kulinda mbuga kama vile Mbuga ya Taifa ya Penjaari nchini Benin au ya Tamdao huko Vietnam.Sasa tumewaleta vijana kutoka maeneo hayo yanayolindwa ili wao pia waweze kutoa mchango wao katika mkutano wa kimataifa unaoendelea mjini Bonn juu ya uhai anuai- yaani njia za kulinda mazingira na viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka."

Vijana wote waliokutana kambini wanashiriki katika miradi ya kuhifadhi mazingira,mimea na viumbe hai nyumbani kwao.Kila mmoja wao alikuwa na hamu kubwa ya kushiriki katika mkutano wa Bonn na mchango wa vijana hao ulikuwa mkubwa na hivyo ilikuwa vigumu mno kuchagua mapendekezo ya kuwasilishwa Bonn.Kila siku vijana hao walihudhuria karakana zilizosimamiwa na waajiriwa wa Mbuga ya Taifa ya Bavaria na wataalamu wa shirika linalotoa misaada ya kiufundi GTZ.Vijana walisaidiwa kutayarisha michezo,kazi za usanaa pamoja na ujumbe wao wa kisiasa, kufikishwa mbele ya mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn.Kijana Reagan anaetoka Namibia ana hakika kuwa atarejea nyumbani na maarifa yenye manufa.Akaongezea:

"Sote tunaishi ulimwengu mmoja.Matatizo ya mazingira nchini Namibia kama vile mashamba kulimwa bila ya kupumzishwa pamoja na ongezeko la joto yanahitaji ufumbuzi.Zipo nchi zilizoshughulikia baadhi ya matatiizo hayo.Kwa kushiriki katika mkutano huo,tumeweza kupeana mawazo na kuelezana hatua zinazochukuliwa nyumbani na kwengineko."

Wakati huo huo mwanafunzi wa Kijerumani,Birgit aliehudhuria mkutano wa vijana wenzake katika Mbuga ya Taifa ya Bavaria amefurahi kupata nafasi ya kubadilishana maoni na kutambua jinsi mimea na viumbe hai vinavyotoweka,au anasema,asingeyaona hayo.Amesema:

"Sisi hatuwezi tena kutimiza mahitaji yetu ya chukula,hivi sasa tunaagizia chakula kingi kutoka nje.Ni muhimu kuelewa kuwa uhai anuai,chakula na usalama wa chakula ni mambo yanayotegemeana.Hapo kabla sikufahamu hayo,lakini sasa suala hilo linanivutia sana."

Kijana huyo wa Kijerumani anasema, wanasiasa wanapaswa kutambua kuwa vijana ni taifa la kesho na wanataka kuhifadhi mazingira kuliko hao wanasiasa, kwani ni vijana watakaokuja kuathirika.Ni matumaini yake kuwa wanasiasa watatambua ukweli huo wa mambo.