Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya waanza | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya waanza

Wakati huu, viongozi wa nchi 27 za Umoja wa Mataifa wanaanza mkutano wao wa siku mbili mjini Brussels. Hali halisi ni tete kati ya wanachama, hasa juu ya mkataba mpya wa Umoja huo.

Angela Merkel anakamilisha muda wake kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya

Angela Merkel anakamilisha muda wake kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya

Siku kumi tu zimesalia hadi pale Ujerumani itakapoipisha ureno kuwa uwenyekiti wa Umoja wa Ulaya. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alikuwa na malengo makubwa ambayo alitaka kuyafikia katika muda huu wa kuuongoza Umoja huu, lakini inaonekana kama muda hautamtosha. Kwani hasa, Bi Merkel alitaka kuanzisha juhudi za kupitishwa mkataba mpya kwa ushirikiano huu wa nchi za bara la Ulaya. Kwenye mkutano huu wa mwisho utakaoongozwa na kansela wa Ujerumani, aliwataka viongozi wenzake wakubali marekebisho yaliyofanywa kuhusiana na katiba ya Ulaya. Hata hivyo lakini, wapinzani hawataki kubadilisha misimamo yao.

Poland ikiwa ni mpinzani mkali zaidi inapinga hasa mfumo mpya wa kupiga kura. Kipya katika mfumo huu ni kwamba unazingatia idadi ya raia. Hivyo, nchi kubwa yenye raia wengi itapata uzito zaidi katika kupiga kura. Ndiyo maana, Poland inahofia kupoteza ushawishi katika Umoja wa Ulaya. Kabla ya mkutano wa leo, viongozi kadhaa wa Umoja wa Ulaya walijaribu kuwashawishi rais na waziri mkuu wa Poland wakubali masharti yalivyo ambayo yanaungwa mkono na nchi 25 kati ya nchi 27 wanachama. Lakini juhudi hizo za kupatanisha hazikuleta mafanikio.

Wapoland wenyewe wana misimamo tofauti juu ya suala hilo. Wengine wanawaunga mkono viongozi wao, wengine wakihofia kutengwa katika Umoja wa Ulaya. Haya ni baadhi ya maoni kutoka Poland:

“Nadhani tishio hilo ni kosa kubwa. Wenzetu katika Umoja wa Ulaya hawataweza kutuamini tena, watatuhofia. Ombi langu ni kwamba hakutakuwepo kura ya turufu, kwani matokeo kwa upande wetu yatakuwa mabaya sana.”
“Je, tunataka Umoja wa Ulaya uchukue uamuzi wake kwa njia ya kidemokrasi au kwa kulazimisha. Mvutano huu si juu ya idadi tu, bali tunapigania nafasi ya Poland ndani ya Umoja huu.”

Uingereza pia ina wasiwasi juu ya mkataba huu mpya. Waziri mkuu Tony Blair alionya kupiga kura ya turufu ikiwa mkataba huo utaingilia sheria za Uingereza na uhuru katika sera za kuelekea nchi za kigeni. Akijibu madai hayo, waziri mkuu wa Luxemburg, Jean-Claude Juncker, alisema: “Tunayo mashairi ya kutosha barani Ulaya. Tunachokihitaji ni sheria na sidhani kwamba nchi ambayo ni moja kati ya muasisi wa demokrasia inataka kuwanyima raia wake faida ya sheria hizo.”

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, José Manuel Barroso, alionya kukubaliana kwa gharama ya juu. Alisema, Umoja wa Ulaya wenye wanachama 27 haupaswi kuwa na sheria hizo hizo za enzi ya wanachama 12 tu. Kwenye mkutano wa kuandaa mazungumzo ya leo, Barroso aliwakumbusha viongozi wa nchi wanachama kuwa lengo si kuipa serikali ya Umoja nguvu zaidi kuliko serikali za kitaifa, lakini ni kuiwezesha Ulaya kufanya kazi vizuri zaidi na kwa demokrasia. Mazungumzo yatakuwa magumu na marefu, lakini suluhisho litapatikana, alisema Barroso.

Suala la mkataba wa Umoja wa Ulaya litazungumzwa leo jioni. Baadaye usiku, Kansela Merkel wa Ujerumani anatarajiwa kuwaarifu waandishi wa habari juu ya matokeo ya siku hii ya kwanza.

 • Tarehe 21.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCP
 • Tarehe 21.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCP
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com