Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya umemalizika. | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya umemalizika.

Mkutano wa kilele wa nchi za Umoja wa Ulaya umemalizika bila ya kuchukuliwa maamuzi juu ya Mkataba wa Lisbon.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani(kushoto) na Rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose' Manuel Barroso.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani(kushoto) na Rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose' Manuel Barroso.

Katika mkutano wao wa jana na leo, viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wameahirisha kuchukuwa uamuzi kutokana na matokeo ya kura ya maoni iliopigwa wiki iliopita na wananchi wa Jamhuri ya Ireland walioukataa Mkataba wa Lisbon unaotaka umoja wao ufanyiwe marekebisho. Sasa kuna hali ya kutokubaliana kuhusu nchi ambazo zimeomba kuingizwa ndani ya Umoja huo- jee uko au hakuna msingi kwa nchi hizo kuingizwa kama wanachama?

Risala kutoka mkutano huo wa mjini Brussels ni wazi, nayo ni kwamba viongozi hao wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya hawajuwi la kufanya na wameahirisha kuzungumzia suala muhimu waliokabiliana nalo. Hali hiyo haiwapi raia, na hasa wananchi wa Jamhuri ya Ireland, imani kuelekea viongozi wao wa Ulaya. Kuliahirisha jambo hilo hadi Oktoba au Disemba yadhihirisha udhaifu wa viongozi hao. Vipi mkataba huo wa Lisbon, ambao unahitajiwa sana, utaweza sasa kukubaliwa na nchi zote 27 ni jambo la kuwekewa alama ya kuuliza. Huenda yakaupata mkataba huu kama yale yalioipata katiba ya Umoja wa Ulaya miaka mitatu iliopita, ambapo, kutokana na upinzani wa Ufaransa na Uholanzi, ilipigwa teke na mwishowe ikazikwa.


Suali sasa ni kama Umoja wa Ulaya, kwa msingi wa Mkataba wa Nizza, unaweza ukaendelea kutojuwa unafanya nini. Jibu ni kwamba unaweza, kwani kinachokosekana katika Umoja wa sasa wa Ulaya sio ratiba inayofanya kazi ya kuchukuwa maamuzi, lakini zaidi kunakosekana nia ya kisiasa ya kusonga mbele kuiunganisha Ulaya na kuendesha siasa ya pamoja. Ni serekali za kila taifa ambazo lazima zioneshe nia hiyo ya kisiasa. Pale mtu anapotaka kuendeleza mradi maalum, basi mtu huyo ataweza kuigundua njia ya kisheria kwa kupitia Mkataba wa Nizza, Rais wa baadae wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Nicolas Sarkozy, anaitegemea njia hiyo. Anataka kuyafikia malengo ya kisiasa katika sekta za nishati, uhamiaji na ulinzi kupitia au kutopitia Mkataba wa Lisbon. Suali ni kama wakuu wa nchi watakubaliana naye au kama yeye ataendelea kujificha nyuma ya mizozo hii ya taasisi na mikataba.


Mkataba wa Lisbon si dawa ya uchawi itakayoondosha mara moja nakisi zilioko ndani ya Jumuiya ya Ulaya. Ikiwa nchi za Jumuiya ya Ulaya zinaona ni muhimu kuwa na rais wa kudumu au waziri wa pamoja wa mambo ya kigeni, basi jambo hilo halihitaji mkataba mkubwa, watu hao wanaweza kupewa nyadhifa hizo kutokana tu na uamuzi wa nchi 27 wanachama, lakini kukiweko nia ya kisiasa. Suala la haki sawa kwa nchi zote wanachama na msingi wa kuweko kauli ya pamoja katika kukata maamuzi sio mambo yanayouwekea Mkataba wa Lisbon alama ya kuuliza. Mtu anaweza akawa na furaha bila ya kuwa na Mkataba wa Lisbon na kuigeuza siasa ya Ulaya, pale nchi zote zinapotaka.


Ugumu utakuweko pale zitakapotaka kuingizwa nchi mpya kama wanachama. Baada ya Mkataba wa Nizza idadi ya juu kabisa iliowekwa kwa wanachama ni 27. Lakini Ufaransa, Ujerumani, Austria, Slovenia na nchi nyingine zinataka, hata bila ya mkataba wa Lisbon, kuzikaribisha nchi nyingine za eneo la Balkan katika klabu hiyo. Hivyo, kuna hatari ya kutokea mabishano makali, kila pale ile tarehe iliopangiwa Croatia kuingizwa, mwaka 2010, inapokaribia. Hapo tena kutaweza kuzuka majadiliano ya kimsingi kama Jumuiya ya Ulaya haitoweza kujilemaza ikiwa itajipanuwa kila wakati na kufikia hadi nchi 34.


Hapo tena ile fikra ya Ulaya inayokwenda kwa kasi za aina mbili inaweza kuzuka na kutekekelezwa kikweli. Pale nchi za eneo la Balkan na baade Uturuki zitakapopewa hadhi ya kuwa washirika wa Jumuiya ya Ulaya, hapo mtu kwa hakika anakuwa na Jumuiya ya tabaka mbili. Tabaka ya tatu au daraja ya tatu ya kasi inaweza ikaziingiza nchi kama vile Ukraine, Georgia au Moldavia, ambazo nazo zinataka ziwemo ndani ya Jumuiya ya Ulaya. Na hata kama viongozi wa nchi mnamo miaka miwili kutoka sasa wataweza kweli kumaliza zoezi hili la kuupatia kibali Mkataba wa Lisbon, bado yatabakia majadiliano juu ya wapi inaishia mipaka ya Jumuiya ya Ulaya.
 • Tarehe 20.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ENb3
 • Tarehe 20.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ENb3
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com