1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya mjini Bruxelles

Oummilkheir22 Juni 2007

Njia bado ni ndefu na imejaqa miba hadi maridhiano yatakapofikiwa kuhusu waraka mpya wa Umoja wa ulaya

https://p.dw.com/p/CB3O
Kansela Angela Merkel ,waziri wa mambo ya nchi za nje Steinmeier na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Barroso
Kansela Angela Merkel ,waziri wa mambo ya nchi za nje Steinmeier na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya BarrosoPicha: AP

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaendelea na duru ya pili ya mazungumzo yao hii leo baada ya duru ya jana usiku kushindwa kuleta tija hasa katika suala la waraka mpya unaotakiwa kua badala ya katiba ya Umoja wa ulaya.

Kikao cha jana usiku cha viongozi wa mataifa 27 ya umoja wa Ulaya kilimalizika bila ya maafikiano na kansela Angela Merkel ,mwenyekiti wa zamu wa Umoja huo alikiri “ masuala ni tete lakini hakuna aliyeonyesha ishara hataki maridhiano yafikiwe”.Kansela Merkel anasema:

“Nia ya kufikia makubaliano iko,hakuna aliyetamka,sitaki mie kesho makubaliano yafikiwe,lakini bado kuna masuala ambayo yanahitaji majibu na mengineyo ambayo ni tete.”

“ Tunataka kuendelea na mazungumzo yetu ya pande mbili pamoja na wawakilishi wa Poland,Uengereza , Uholanzi na jamhuri ya Tcheki pia” amesema kansela Angela Merkel alipowasili katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya hii leo.Alikutana tena na rais Lech KACZYNSKI wa Poland,baada ya mazungumzo yao ya jana usiku.Safari hii walishiriki pia rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na rais wa Lithuania Valdas Adamkus.

Baada ya chakula cha mchana,viongozi wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kukutana tena kuzungumzia waraka mpya unaotazamiwa kuchukua nafasi ya katiba inayobishwa ya Umoja wa ulaya..

Ndugu wawili mapacha Kaczynski wanaoiongoza Poland hivi sasa- wanapinga utaratibu wa “wingi mara dufu wa kura” katika kupitishwa maamuzi ya Umoja wa Ulaya na kufika hadi ya kudai wapoland waliouliwa na wanazi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia wazingatiwe kua ni sehemu ya wananchi wao.Hoja hizo zimezusha ghadhabu miongoni mwa viongozi wengine wa Ulaya.Spika wa bunge la Ulaya Hans-Gert Pöttering anasema:

“Matamshi kama hayo yanaumiza na hayastahiki kutolewa katika karne hii ya 21.”

Rais Nicolas Sarkozy amependekeza mpango badala, mfano wa ule uliofikiwa na Umoja wa Ulaya mjini IOANNINA nchini Ugiriki mwaka 1994 ili kundi dogo la nchi liwe na haki ya kudai uamuzi udurusiwe upya licha ya kupitishwa kwa wingi unaohitajika.

Waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair nae pia anashikilia madai ya nchi yake yazingatiwe kikamilifu.Uengereza inapinga sheria msingi na fikra ya kuchaguliwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya. Wafaransa,wahispania na wataliana wamesema watajitahidi kutuliza hofu za Uengereza wakisema watakua tayari kuridhia Muongozo wa haki za kimsingi usiwe jambo la lazima kufuatwa nchini Uengereza.

Lakini nchi hizo tatu haziko tayari kuachia fikra ya kubuniwa wizara ya mambo ya nchi za nje ndani ya Umoja wa ulaya japo kama hawashikilii muakilishi huyo aitiwe “waziri “kama inavyotajwa ndani ya katiba.

Ili kusaka ufumbuzi wa mivutano yote hiyo,kansela Angela Merkel anaendelea na mazungumzo ya pande mbili pamoja na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Duru za ujumbe wa Poland zinasema Warsaw imetoa mapendekezo mepya kujibu yale yaliyotolewa na rais Sarkozy wa Ufaransa.

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya,wa mwisho chini ya usimamizi wa kansela Angela Merkel utaendelea baada ya chakula cha mchana hii leo.