1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa NATO waanza

Admin.Lilian Mtono8 Julai 2016

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO umeanza mjini Warsaw, huku Rais Barack Obama akiwataka viongozi hao kusimama imara dhidi ya kuibuka upya kwa Urusi na kutotikiswa na Uingereza kujiengua Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1JLjW
NATO Gipfel in Warschau Treffen an die Marginen Obama mit Tusk und Juncker
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Katika makala yake kwenye jarida la Financial Times iliyochapishwa leo, muda mchache kabla ya kuanza mkutano huo wa kilele, Obama amewataka viongozi wa Ulaya kusimama thabiti dhidi ya hatua ya Urusi ya kuutwaa mkoa wa Crimea uliokuwa sehemu ya kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, na changamoto nyingine zinaikabili jumuiya hiyo ya kiusalama, hasa katika kipindi hiki ambacho Uingereza inatishia kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, ikulu ya Urusi, Kremlin, imetoa taarifa yake ikisema kuwa inatazamia akili ya kawaida itatawala kwenye mkutano huo wa kilele wa NATO, na ikitupilia mbali hoja ya NATO kuichukulia Urusi kuwa ni kitisho kwao.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema Urusi imekuwa na itaendelea kuwa tayari kwa majadiliano na NATO wakati wowote na pia kushirikiana nayo.

Rais Obama aliyewasili katika mkutano wake huo wa mwisho wa NATO kabla ya kuachia madaraka, amesema anaamini kwamba kujitoa kwa Uingereza, kutaifanya Jumuiya hiyo ya kujihami kuwa kiungo muhimu zaidi cha kuwaunganisha wanachama waliosalia wa umoja wa Ulaya.

Rais Barack Obama alipofungua mkutano huo
Rais Barack Obama alipofungua mkutano huoPicha: Reuters/J. Ernst

"Ninaamini kwamba mataifa yetu yatatakiwa kukusanya nguvu ya kisiasa na kuwa na msimamo thabiti katika kukabiliana na changamoto zilizopo. Naamini tunaweza, lakini tu iwapo tutasimama pamoja kama washirika wamoja" Obama aliandika.

Matamshi ya Obama yametolewa ijumaa hii baada ya kufungua mkutano wa siku mbili unaowakutanisha viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa jumuiya ya kujihami ya NATO, unaofanyika mjini Warsaw, Poland. Obama alifanya ufunguzi huo pamoja na rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk na rais wa kamisheni ya umoja huo, Jean-Claude Junker.

Mataifa 28 ya Jumuiya hiyo Ijumaa hii watakubaliana rasmi kupeleka vikosi vinne vya wanajeshi vitakavyokuwa na askari kati ya 3000 hadi 4000 katika mataifa ya Baltiki na Poland ya Magharibi, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kawaida wa kuhakikisha utayari wake wa kuwalinda wanachama wake wa Magharibi.

NATO Gipfel in Warschau Veranstaltungsort
Picha: DW/B. Riegert

Licha ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kuonekana kupuuzia hali ya wasiwasi iliyotawala mkutano huo, atahudhuria mkutano kati ya Urusi na NATO wiki ijayo, huo ukiwa ni mkutano wa pili ulioshinikiza Urusi kuiachia Crimea mnamo mwaka 2014. Urusi iliyaruhusu makubaliano yaliyofikiwa na Umoja wa Mataifa yaliyotoa mamlaka kwa Umoja wa Ulaya kuingilia biashara ya silaha zilizopelekwa Libya kupitia bahari ya Mediterania.

Katibu Mkuu huyo ameelezea imani yake kwamba kujiondoa kwa Uingereza ya kwenye Umoja wa Ulaya, hakutaathiri mahusiano na Marekani, na kusema kuwa Uingereza bado itaenedelea kuwa mwanachama hai kwenye Jumuiya hiyo ya kiusalama.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef