Mkutano wa hali ya hewa Bonn waendelea | Masuala ya Jamii | DW | 08.06.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mkutano wa hali ya hewa Bonn waendelea

Mkutano wa kimataifa wa watalaama wa hali ya hewa na mazingira, unaendelea hapa Bonn, huku, wanaharakati mbalimbali wa masuala ya mazingira wakijaribu kuwasilisha mapendekezo yao.

default

Watalaam hao zaidi ya elfu 3 kutoka nchi zipatazo 190 wanajaribu kufungua njia ya kufikiwa kwa mkataba mpya wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, mkataba ambao unatarajiwa kutiwa saini mwezi Desemba mwaka huu mjini Copenhagen Denmark, kuchukua nafasi ya ule wa Kyoto.


Kundi linajumuisha baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya umoja huo, yanayoudhuria mkutano huo, leo yametoa wito wa kutaka kujadiliwa kwa suala la majanga ya kibinanadamu yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.


Kundi hilo linalojumuisha mashirika zaidi ya 18 limesema kuwa ni muhimu kwa majadiliano hayo kutilia maanani majanga ya kibinaadamu yanasababishwa na mabadiliko hayo ya hali ya hewa, na kwamba liwemo katika rasimu ya mkataba mpya utakaochukua nafasi ya ule wa Kyoto.


Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinaadamu, John Holmes amesema kuwa, kiwango cha majanga ya kibinaadamu yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika siku zijazo ni kikubwa, na kwamba ni lazima kuchukuliwa kwa hatua mujarabu kupunguza kiwango hicho.


Kwa mujibu wa utafiti uliyofanywa na taasisi ya wakimbizi ya Norway kwa kushirikiana na ofisi ya masuala ya kibinaadamu OCHA, zaidi ya watu millioni 20 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na majanga ya kibinaadamu yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali hewa.


Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya Norway Elisabeth Rasmusson amesema kuwa idadi ya watu wanaolazimika kuwa wakimbizi kutokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa imeongezeka sana


´´Majanga ya kiasili ni miongoni mwa mambo makuu yanayowalazimisha watu kuyahama makaazi yao na mamilioni ya watu wamekumbwa na hali hiyo.Utafiti wetu umebaini kuwa katika kipindi cha mwaka 2008 pekee zaidi ya watu millioni 20 wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na majanga ya kiasili yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mafuriko na dhoruba´´


UN Klimasekretär Yvo de Boer

Katibu Mkuu UNFCCC Yvo de Boer

Naye Katibu Mkuu wa Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulika na mabadiliko ya hali ya hewa,UNFCCC, Yvo de Boer pamoja na kuelezea matumaini yake katika kufikiwa kwa makubaliano mwisho mwa majadiliano hayo, lakini amesema kuna baadhi ya masuala ambayo ni muhimu kuwekwa wazi kwani yatarahisisha mchakato wa kufikiwa kwa mkataba mpya katika mkutano wa Copenhagen.


´´Nadhani tunahitaji uwazi katika malengo ya nchi binafsi, kupunguza kiwango cha utoaji wa gesi inayoharibu mazingira, hususan kwa nchi zilizoendelea kiviwanda, kwasababu bila ya hivyo hakuna lolote litakalofanyika .Pia lazima kwa nchi zilizoendelea kuainisha wazi hatua ilizozichukua kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa, hususan kwa mataifa yale yanayojulikana kama mataifa muhimu yaliyoendelea´´


Aidha Bwana de Boer ametahadharisha kuwa iwapo hakutafikiwa makubaliano ya mkataba mpya basi dunia itakuwa kwenye hatari kubwa, huku watu millioni 250 barani Afrika wakiwa katika hatari kubwa ifikapo mwaka 2020.


Hata hivyo amesema kuwa mchango wa Afrika katika majadiliano hayo ni mkubwa.

Nchi za kiafrika zimekuwa na mchango muhimu, na kabla ya mkutano huu mawaziri wa kiafrika walikutana mjini Nairobi kuamua nafasi ya Afrika katika majadiliano haya, na kwa kweli Afrika imekuwa ikisisitiza sana katika majadiliano haya kuwa mabadiliko katika matumizi ya nishati kutokana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa ni muhimu sana kwao´´


Mkutano huu wa Bonn unatarajiwa kukamilika Ijumaa hii baada ya wiki takriban tatu za majadiliano.


Mwandishi:Aboubakary Liongo/Klima Konferenz Bonn

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com