Mkutano wa G8 Heiligendamm unaanza | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mkutano wa G8 Heiligendamm unaanza

Viongozi wa madola manane tajiri wamekusanyika kwenye mji wa mwambao wa Heiligendamm kaskazini mwa Ujerumani kwa mkutano wa kilele wa G-8.

default

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya,ataongoza mkutano huo wa kilele unaokabiliwa na mivutano kati ya Marekani na Urusi pamoja na suala la ongezeko la joto duniani.

Inasemekana kuwa sasa Kansela Merkel wa Ujerumani na Rais George W.Bush wa Marekani wameonyesha dalili za kuafikiana juu ya suala linalohusika na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Juu ya hivyo lakini viongozi hao bado wanatofautina sana katika suala hilo.Inatazamiwa kuwa wakati wa chakula cha mchana viongozi hao wawili wataweza kuondosha tofauti zao kabla ya mkutano wa kilele wa G-8 kufunguliwa rasmi baadae leo hii mjini Heligendamm.

Wakati Marekani imekiri kuwa ongezeko la ujoto duniani ni tatizo kubwa,nchi za Ulaya sasa zinakubaliana na maoni ya Marekani kwamba hakutokuwepo suluhisho la maana bila ya kushiriki kwa nchi zinazoinukia kiuchumi na kutumia nishati kwa wingi kama China,India na Brazil.Wakati huo huo wanakubaliana kuwa ukuaji wa uchumi hauwezi kuwa muhanga wa mipango ya kulinda mazingira.

Lakini Kansela Merkel anahofu kuwa mivutano kati ya Bush na Putin huenda ikagubika mada zingine mkutanoni kama vile mabadiliko ya hali ya hewa duniani na misaada kwa bara la Afrika.Kwani Rais Bush siku ya Jumanne,aliikosoa Urusi kuhusu suala la demokrasia.Bush alikuwa akizungumza Prague mji mkuu wa Jamhuri ya Czech kabla ya kwenda Heiligendamm.Hapo hapo alijaribu kumtuliza Putin kuhusu mradi wa Marekani wa kutaka kuweka baadhi ya makombora yake ya kinga nchini Poland na Jamhuri ya Czech.Amemuambia Putin kuwa hana cha kuhofia kwani mradi huo ni wa kujihami tu.Juu ya hivyo,Rais Putin amesema,pindi Washington itaendelea na mpango wa kuweka makombora barani Ulaya,basi Urusi itachukua hatua ya kuanza kuyaelekeza makombora yake Ulaya,kama ilivyokuwa enzi ya Vita Baridi.

Lakini hilo si suala pekee lililosababisha mivutano kati ya Marekani na Urusi.Kwani serikali ya Moscow vile vile inapinga pendekezo la Marekani na nchi za Ulaya la kutaka kulipa uhuru, jimbo la Kosovo lililojitenga na Serbia.

Hata hivyo,ni matumaini ya Kansela Merkel kuwa kwenye mkutano wa Heiligendamm utakaoendelea hadi tarehe 8 Juni maafikiano yataweza kupatikana kuweka malengo ya kupunguza gesi zinazochafua mazingira kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2050.Lakini kuna shaka kama Marekani itaweza kushawishiwa kukubaliana na malengo thabiti kama hayo.Kwani matamshi ya Bush ya juma lililopita,yamezusha wasi wasi kuwa Marekani huenda ikafuata njia yake yenyewe badala ya kufuata utaratibu uliokwishawekwa na Umoja wa Mataifa kuhusika na hatua za kuchukuliwa kupunguza gesi zinazoathiri mazingira.

Kwa mujibu wa wataalamu wa sayansi ikiwa hatua hazitochukuliwa,viwango vya usawa wa bahari vitapanda juu na vile vile ukame na mafuriko duniani yataongezeka.

Juu ya tofauti za maoni zilizokuwepo,maafisa wa Marekani na Ujerumani wamesema,wanaamini kuwa makubaliano ya pamoja yatapatikana kwenye mkutano wa Heiligendamm.

Kwa upande mwingine,maelfu ya wanaharakati walioazimia kuandamana kupinga mkutano wa G-8 wameweza kuvikwepa vizuizi vya polisi na kuelekea sehemu kunakofanywa mkutano huo.Wakati huo huo makundi ya kiraia yanayoukubali mkutano wa G-8, lakini wakitaka kuwashawishi viongozi wa Magharibi kuongeza misaada barani Afrika wametayrisha maandamano ya amani na wanahudhuria mkutano mbadala wa kilele,mjini Rostock.

 • Tarehe 06.06.2007
 • Mwandishi Prema Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB3l
 • Tarehe 06.06.2007
 • Mwandishi Prema Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB3l

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com