1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa CEN-SAD wamuunga mkono al-Bashir

23 Julai 2010

Rais Deby wa Chad asema waranti dhidi ya Bashir zinavuruga mchakato wa amani Darfur.

https://p.dw.com/p/OSGe
Rais Bashir wa Sudan anatuhumiwa na mahakama ya ICC kwa makosa ya mauaji ya halaiki, DarfurPicha: dpa

Mkutano wa kanda unaoendelea nchini Chad umemuunga mkono rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir anayetuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki, ukisema kwamba unazipuuza ‘tuhuma zote’ dhidi yake. Wakati huo huo, rais wa Chad, Idriss Deby katika hotuba aliyotoa mbele ya viongozi wa jumuiya ya mataifa ya ukanda wa Sahel wa jangwa la Sahara CEN-SAD, aliwataka viongozi wenzake wasaidie kuleta suluhisho katika mzozo wa Darfur.

Kiongozi wa Jumuiya hiyo ya mataifa ya ukanda wa Sahel, CEN-SAD, Mohammed al-Madani al-Azhari amesema jimbo la Darfur linaendelea kuwa chanzo cha wasiwasi na kwamba jumuiya hiyo inapinga madai yote dhidi ya Rais Bashir na ni tuhuma ambazo hazisaidii katika kuleta amani katika eneo hilo la Sudan. Akizungumza mbele ya viongozi wa nchi 13, alisema kwamba ni wazi wanaiunga mkono na kuonyesha mshikamano wao na nchi ya Sudan na raia wake.

Friedensvertrag zwischen Tschad und Sudan, Omar al-Bashir, Idriss Deby, Freies Bildformat
Rais Bashir wa Sudan na mwenyeji wake rais Idriss Deby nchini Chad.Picha: picture-alliance/ dpa

Ziara hiyo ya rais Bashir ni ya kwanza katika nchi ambayo inaitambua mahakama ya uhalifu wa kivita ilioko 'The Hague', Uholanzi na Chad imekosolewa vikali na Jumuiya ya Ulaya na mashirika ya kutetea haki za binaadamu kwa kukataa kumkamata Rais al-Bashir.

Rais Deby aliukaribisha mchango wa jumuiya hiyo ya CEN-SAD katika kuleta amani barani Afrika na kwamba katika mfumo huo, lazima wasaidie katika mchakato wa mazungumzo ya amani ya Doha, Qatar kati ya serikali ya Sudan na waasi wa jimbo la Darfur.

Kundi kuu la waasi katika jimbo la Darfur liitwalo ‘Justice and Equality Movement’ , JEM ilisaini makubaliano ya amani mwezi Februari mjini Doja yaliyotajwa na Jumuiya ya kimataifa kama hatua muhimu ya kuleta amani katika eneo lililozongwa na vita vya miaka saba. Hata hivyo hakukuwa mkataba thabiti wa amani na muda wa mwisho wa tarehe 15 mwezi Machi ulipotimia, Kundi hilo la JEM lilisusia mazungumzo hayo na kurudi tena vitani.

Msemaji wa wizara ya ndani ya Marekani, Phillip Crowley alisema mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani nchini Chad alizungumza na viongozi nchini humo kuhusu ziara ya Bashir na akasema ushirikiano kati ya Sudan na Chad wa hivi karibuni ni maendeleo mazuri na kwamba ukiendelea maisha ya watu yataokolewa katika eneo la Darfur.

Bw Crowley alisema wamewasiliana na taifa hilo kwamba inawajibika kama mwanachama wa mkataba wa Roma na inahitaji kuendelea kuyatimiza majukumu yake chini ya mapendekezo ya mahakama ya ICC.

Milizen im Darfur
Waasi katika jimbo la Darfur. Vita vya tangu 2003 vimesababisha vifo vya raia laki tatu.Picha: picture-alliance/ dpa

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, Darfur eneo ambalo ni jangwa, lenye ukubwa sawa na Ufaransa limekumbwa na vita tangu mwaka wa 2003 vilivyosababisha vifo vya kiasi ya watu laki tatu na kuwaacha wengine milioni 2.7 bila makaazi.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed