1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mkutano wa baraza la taifa China waanza leo

Angela Mdungu
5 Machi 2021

Mkutano wa baraza la taifa la China (NPC) ni tukio kubwa zaidi la kisiasa nchini humo. Katika ajenda ya mwaka huu ni mabadiliko yakijani ya kiuchumi  wakati China ikiendelea kukua kama taifa lenye nguvu duniani

https://p.dw.com/p/3qFVk
China Peking | Eröffnung Jahrestagung Volkskongress
Picha: Carlos Garcia Rawlins/REUTERS

Chama cha kikomunisti cha China, wakati mwingine hutumia baraza la taifa kutangaza mabadiliko makubwa ya sera na watumishi. Mkutano wa baraza hilo unaanza leo Ijumaa mjini Beijing. Kwa mwaka wa pili mfululizo, utafanyika kwa njia ya video kutokana na janga lavirusi vya corona.

Ingawa baraza hilo ndilo chombo kikuu cha kutunga sheria, Chama cha kikomunisti huhakikisha kuwa maamuzi muhimu yanafanyika muda mrefu kabla mapendekezo hayajakifikia chombo hicho.

Kati ya mambo yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo utakaodumu kwa siku 10 hadi 14, ni mustakabali wa hali ya uchumi wa Hong Kong.

Nini cha kutarajiwa katika mkutano huu?

China ilifanikiwa kulidhibiti kwa kiasi fulani janga la COVID 19 mapema kuliko nchi nyingine. Ilihakikisha kuwa uchumi unaimarishwa kwa haraka. Lakini bado madhara ya janga hilo katika uchumi wa dunia na muendelezo wa mgogoro kati ya taifa hilo na Marekani vinamaanisha kuwa makampuni ya taifa hilo yanakabiliwa na hali ya sintofahamu.

Kwa maafisa mipango wa uchumi wa China, kuimarisha matumizi na mahitaji ya ndani vinabaki kuwa mambo muhimu ya kuhakikisha maendeleo endelevu.

Mtafiti katika taasisi ya MERICS ya China yenye makao yake mjini Berlin, Caroline Meinhardt anasema suala hili lina nafasi kubwa. Lakini kufuata mkakati kutamaanisha kuwa serikali inakabiliwa na changamoto ya muda mrefu. Hii ni kwasababu kuimarisha ukuaji katika mahitaji kunataka mgawanyo mkubwa wa vipato katika kaya za kawaida.

Asien I China I Neujahr I LUNAR
Rais wa China Xi JinpingPicha: Ju Peng/Xinhua/picture alliance

Naye mtafiti anayefanya kazi na Meinhardt anasema katika miaka ijayo lengo kuu litakuwa ni kuimarisha uchumi wa nchi na viwanda, kutanua mifumo ya kijamii hasa katika sekta za afya na elimu.

Eneo jingine la kutizamwa zaidi litakuwa ni kukuza vumbuzi wa ndani na kuwekeza katika teknolojia kwa ajili ya baadaye. Mgongano wa kibiashara kati ya Marekani na China, umeonesha wazi udhaifu wa China hasa katika utegemezi wake mkubwa kwenye usmabazaji wa bidhaa zinazotumia teknolojia ya hali ya juu.

Meinhardt anasema, kwa sasa China bado iko mbali na kuwa huru kiteknolojia. Unafuu pekee unatokana na uungaji mkono wa hali ya juu wa serikali na uwekezaji binafsi na hii huenda ikaifanya China kupata mafanikio makubwa kwenye sekta ndogo ndogo katika miaka ijayo.