Mkutano mkuu wa Republican huko Marekani wamchagua McCain kama mtetezi wa urais | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano mkuu wa Republican huko Marekani wamchagua McCain kama mtetezi wa urais

McCain ni mtetezi wa urais katika uchaguzi ujao wa Marekani

John McCain pamoja na mgombea wake mwenza. Sarah Palin

John McCain pamoja na mgombea wake mwenza. Sarah Palin

John McCain amekubali kuwa mtetezi wa chama chake cha Republican kwa uchaguzi wa urais wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu, akiahidi kwamba mabadiliko yatakuja mjini Washington baada ya kipindi cha sasa cha Rais George Bush. Alisema si mshindani wake, Barack Obama wa Chama cha Democratic, lakini ni yeye atakayeleta mabadiliko. John McCain aliufunga jana usiku mkutano mkuu wa Chama cha Republican huko St. Paul, katika mkoa wa Minnesota, akishangiliwa na maelfu ya viongozi wa chama hicho, wengi wao hapo kabla hawajakuwa wakipendezwa na misimamo yake ya kujitegemea.

John McCain alisema hapo kabla alifanya kazi na maseneta wa Chama cha Democratic, mara nyingi Wa-Republican wakiudhika, lakini pindi atachaguliwa kuwa rais ataendelea kufanya vivyo hivyo. Alitoa mwito mbele ya wajumbe 20,000 wa chama chake kukomeshwe mabishano yasiokwisha baina ya vyama hivyo viwili vya Democratic na Republican. Bila ya shaka, hilo lilikuwa ni jaribio kutaka kupata kura za watu wanaojitegemea na za Wa-Democratic, kura ambazo ni muhimu kwake, ikiwa ashinde. Pia ilikuwa ni ishara ya tafauti baina ya vyama vya Democratic na Republican kuhusu siasa ya Marekani kuelekea vita vya Iraq.

Mwanasiasa huyo, mwenye umri wa miaka 72, na shujaa wa vita, aliahidi atapigana kwa ajili ya Marekani kwa muda wote atakapokuwa anavuta pumzi, akihoji kwamba tabia alioipata kwa kuwa vitani huko Vietnam imempa nguvu za kuamua na kuwa na upeo wa mbali wa kuona mambo, hivyo kuweza kuongoza kama rais. Alisema Wamarekani wanakabiliana na vitisho vingi katika dunia hii ya hatari, lakini yeye haogopi. Aliwaambia Wamarekani wasiufumbie macho uchokozi na vurugu za kimataifa zisizojali sheria na ambazo zinahatarisha usalama na utulivu wa dunia pamoja na usalama wa Wamarekani

John McCain, ambaye anasifika kwa kuwakaripia hata viongozi wa Chama chake cha Republican, aliahidi kwamba yeye na mgombea wake mwenza, Bibi Sarah Palin, watazitikisa kufuli zilizofunga milango ya serekali huko Washington. Alitoa onyo la mapema kwa maafisa wa serekali waliozowea kutumia ovyo fedha za serekali, watu wanaojiangalia wao kwanza na nchi baadae, kwamba mabadiliko yatakuja. Aliongeza kusema kwamba ana heshima kuukubali uamuzi wa mkutano mkuu wa Chama cha Republican kumteuwa yeye kama mtetezi wa urais kwa niaba ya chama hicho.

"Ahsanteni sana. Nimepata hesima na nafasi ambayo Wamarekani wacheche wanapewa, heshima na nafasi ya kukubali kuteuliwa kupigania wadhifa wa rais wa Marekani."

Kinyume na siku ya mwisho ya mkutano mkuu wa Chama cha Democratic, siku kumi zilizopita huko Denver, ambapo Barack Obama alihutubia katika uwanja ulio wazi wa kandanda, mara hii McCain alisimama juu ya jukwaa la kawaida lililoenea hadi kwenye viti vya wajumbe wa mkutano. Hotuba yake iliingiliwa na vifijo na watu waliozomea kila pale alipokuwa anazitaja siasa za chama cha Democratic.

Alisema anamheshimu Barack Obama:

"Kuna mambo mengi yanayotuweka pamoja na Barack Obama kuliko yale yanayotutafautisha."

Lakini wakati wa hotuba ya McCain hakujakuweko shangwe kubwa kama zile zilizomkabili Sarah Palin, mgombea mwenza, alipotoa hotuba yake juzi.

McCain alimtaja rais George Bush mara moja tu, na sio kwa jina, pale alipomshukuru rais huyo ambaye amepoteza imani ya Wamarekani wengi, kwa kuzuwia kutokea mkasa mwengine wa shambulio la kigaidi kama lile la Septemba 11.

McCain alimaliza hotuba yake kwa tamko hili:

" Sisi ni Wamarekani, hatusalimu amri hata kidogo,hatujifichi kutoka historia, sisi ndio tunaofanya historia."

Mkutano huo mkuu uliingiliwa kati na waandamaji wachache waliokuwa wanapinga vita na ambao walipenye ndani ya ukumbi huo


Watu wanaomfanyia kampeni Barack Obama walisema hotuba ya McCain haijawa na lolote jipya, ni maneno yale yale, na haijatoa kitu chochote kipya, mbali na kile ambacho Bush anakifanya sasa.

 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FBw7
 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FBw7
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com