Mkutano mkuu wa chama cha Republican nchini Marekani waanza taratibu. | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.09.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano mkuu wa chama cha Republican nchini Marekani waanza taratibu.

Ni baada ya kufutwa baadhi ya ratiba kushikamana na walioko katika maeneo kulikopita kimbunga cha Gustav

Mkutano mkuu wa chama cha Republican nchini Marekani katika jimbo la Minnesota umeanza taratibu huku kitisho cha kimbunga Gustav nacho pia sasa kikipungua. Mkutano huo uliovunja sehemu kubwa ya ratibayake jana ili kuonyesha mshikamano na walioyahama makaazi yao huko New Orleans kujinusuru na athari za kimbunga hicho,

Miongoni mwa yaliondolewa katika ratiba ya jana ni pamoja na kufutwa hotuba ya Rais George W.Bush aliyekwenda Texas kuangalia shughuli za misaada ya kiutu kutokana na kimbunga cha Gustav.

Hata hivyo kutokuwepo kwake mkutanoni na kukosekana pia kwa makamu wake wa Rais Dick Cheney aliyepangiwa pia kuzungumza, hakuja wazuwia waandamanaji kiasi ya 10,000 walioingia katika ukumbi wa mkutano wakipiga kelele za kupinga vita na mabango yaliokua na maandishi ya kumkosoa Bush na vita nchini Irak. Polisi waliojizatiti vyema na kutumia hewa ya kutoa machozi, waliwatia nguvuni kiasi ya waandamanaji 130.

Hata hivyo mkewe Rais Bush, Bibi Laura Bush na Bibi Ciny McCain mke wa mgombea wa Warepublican John McCain walioongoza kampeni ya kuwachangia fedha wahanga wa kimbunga cha Gustav.

Tukirudi katika mkutano huo wenyewe, wakati ukitarajiwa kuanza alau kupata kasi kuanzia leo, umegubikwa na kile wahenga wanachokiita ndege mbaya. Ukiweka kando kufutwa hotuba ya Rais Bush na Makamu Cheney, mgombea mwenza wa McCain Sarah Palin amegeuka kuwa gumzo la wengi, baada ya kufichua kwamba binti yake Bristol mwenye umri wa miaka 17 ana mimba ya miezi mitano sasa nje ya ndoa.

Bibi Palin ni mpinzani mkubwa wa utoaji mimba na kuchanguliwa kwake na McCain kuwa mgombea mwenza kulilengwa katika kuvutia kura za Warepublican wahafidhina. Hata hivyo kufichuliwa kwa kisa hicho cha binti yake Bibi Palin kumeanza kuzusha masuali mengi miongoni mwa wapiga kura, huku binafsi akiviomba vyombo vya habari viheshimu masuala ya faragha ya familia yake.

Mbali na kisa hicho, mgombea mwenza huyo wa Bw McCain anaendelea kuchunguzwa jimboni mwake Alaska ambako ni Gavana baada ya kumfukuza kazi kamishna wa usalama wa umma aliyekataa kumtimua kazini shemeji yake Bibi Palin.

Anadai shemeji yake huyo aliyekua katika taratibu za kuachana na dada yake Palin, aliitisha familia yake. Uchunguzi wa kisa hicho iwapo alitumia kweli madaraka yake kushawishi uamuzi uliohusiana na suala la kifamilia utatolewa mwezi Oktoba kabla ya uchaguzi wa Rais wa Marekani Novemba 4, wakati McCain atakapopambana na mgombea wa chama cha Democaratic Barack Obama. Wadadisi wanasema kampeni na kupeana changa moto kwa wagombea wa Warepublican na Wademocrats itaanza kupamba moto baada ya mkutano huo wa mkuu wa Warepublican huko St Pauli Minnesota.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com