Mkutano kuhusu usalama wa kinyuklia kufunguliwa leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano kuhusu usalama wa kinyuklia kufunguliwa leo

Mkutano huo utakaowahusisha viongozi wa nchi 46, unafanyika huko Washington, Marekani.

default

Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo.

Wakati Rais Barack Obama wa Marekani leo anatarajiwa kufungua mkutano wa kilele kuhusu usalama wa kinyuklia, Iran, kwa upande wake, imesema itapuuzia maamuzi yoyote yatakayochukuliwa na mataifa yenye nguvu duniani katika mkutano huo wa siku mbili unaofanyika mjini Washington.

Mjumbe wa Iran katika Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki-IAEA, Ali-Asghar Soltanieh, ameliambia shirika la habari la ISNA kuwa maamuzi yatakayofikiwa katika mkutano kuhusu usalama wa kinyuklia hayaifungi Iran. Amesema kuwa wakati Marekani imezingatia misingi ya kuchagua washiriki wa kuwaalika katika mkutano huo, hakuna wajibu kwa nchi ambazo hazijaalikwa kama vile Iran kufuata maamuzi yatakayofikiwa kwenye mkutano huo.

Huku akiituhumu Marekani kwa kutofuata kanuni za kimataifa, Bwana Soltanieh amesema kuwa Israel ni kikwazo kikubwa katika kuzuia kuenea silaha za nyuklia kwa kutouheshimu mkataba wa kuzuia kuenea silaha za nyuklia-NPT. Wiki iliyopita Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alitangaza uamuzi wake wa kutohudhuria mkutano huo.

Bwana Soltanieh amesema Iran ilitia saini mkataba wa NPT na ni mwanachama wa IAEA na kwamba mipango yake ya kinyuklia inafanana na mifumo na kanuni zote za kimataifa. Mjumbe huyo wa Iran kwenye Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki amerudia kusema kuwa Iran iko tayari kurejea kwenye mazungumzo na mataifa yenye nguvu duniani kuhusu miradi yake ya kinyuklia, lakini haitatishwa na vikwazo au hata vitisho vya kijeshi.

Akizungumza jana kabla ya mkutano huo, utakaowashirikisha viongozi wa nchi 46, Rais Barack Obama alielezea uwezekano wa makundi ya magaidi kama vile al-Qaeda kutumia silaha za kinyuklia, ambapo alisema makundi hayo hayatasita kutumia mabomu ya kinyuklia iwapo watayapata na hivyo kuwa ni kitisho kikubwa kwa usalama duniani. Rais Obama alisema, ''Kwa bahati mbaya tuko katika hali ambapo kuna nyenzo nyingi za kinyulia kwenye kila eneo duniani. Na hivyo, lengo kuu la mkutano huu ni kuiweka jumuiya ya kimataifa katika njia ambayo tutaweza kuzuia nyenzo hizi za kinyuklia katika muda maalum kwa mpango maalum.''

Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano huo kuhusu usalama wa kinyuklia, amesema leo kuwa wakati umefika wa kutolewa maamuzi zaidi ya vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kutokana na nchi hiyo kutuhumiwa kutengeneza silaha za kinyuklia.

Akizungumza na waandishi habari kabla ya kuelekea Washington, Bibi Merkel alisema Rais Hu Jintao wa China na Dmitry Medvedev wa Urusi, ambao hadi sasa wanasita kuhusu suala la Iran kuwekewa vikwazo vipya, wote watakuwepo katika mkutano huo na anataka kuona kama nchi hizo mbili zitapiga kura kwa Iran kuwekewa vikwazo au zitatumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Marekani inaongoza jitihada za kutaka Iran iwekewe vikwazo vikali kuhusu mpango wake wa kinyuklia, ambao nchi hiyo na zile nchi washirika wake zinasema kuwa mpango huo wa Iran una lengo la kutengeneza silaha za nyuklia, tuhuma ambazo Iran imekuwa ikizikanusha.

Mwandishi: Grace Patricia kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 12.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Muaz
 • Tarehe 12.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Muaz
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com