1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Syria waanza Cairo

2 Julai 2012

Kiasi ya wajumbe 250 wa upinzani wa Syria wanakutana mjini Cairo, Misri, kwenye mkutano wa kuijadili amani ya Syria ulioandaliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, lakini waasi na wanaharakati wamepanga kuugomea mkutano huo.

https://p.dw.com/p/15Pgf
Mkuu wa upinzani wa Syria, Hassan Abdel Azim.
Mkuu wa upinzani wa Syria, Hassan Abdel Azim.Picha: picture-alliance/dpa

Mkutano huo wa siku mbili unaowashirikisha wapinzani wa utawala wa Syria walioko nje ya nchi hiyo, Baraza la Taifa la Syria, SNC, ambacho ni chombo cha kisiasa cha wapinzani pamoja na makundi mengine, unatarajiwa kutoka na dira ya pamoja kuhusu hatma ya nchi hiyo hapo siku za baadae.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inayosimamia mkutano huo imesema kuwa mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Ufaransa, Tunisia, Uturuki pia wamealikwa kushiriki kwenye mazungumzo hayo kwa kuwa nchi hizo pia zilishiriki kwenye mkutano wa marafiki wa Syria siku za nyuma.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapeleka mwakilishi wake pia kwenye mkutano huo. Msemaji wa SNC anasema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwa na mafaniko na utatoka na ripoti mbili, ya kwanza itaitwa "ahadi za kitaifa za Syria" na ya pili itaitwa "hatua za kipindi cha mpito".

Siku ya Jumamosi mataifa yenye nguvu duniani yalikubaliana kuundwa serikali ya mpito kwenye mkutano uliofanyika mjini Geneva, Uswisi, itakayowajumuisha wajumbe kutoka utawala wa Rais Bashar al-Assad na upinzani.

Wapinzani wasema kuna ajenda ya Iran, Urusi

Wakati washiriki wakiwa kwenye maadalizi ya mkutano huo, tayari waasi na wanaharakati nchini Syria wametangaza kuugomea mkutano huo wakisema kuwa ni aina ya hatua yenye lengo la kuziunga mkono ajenda za Urusi na Iran.

Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan.
Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan.Picha: Reuters

"Hatutashiriki mazungumzo wala mapatano yoyote na makundi ya wauwaji. Na hatutaruhusu mtu yoyote apandikize ajenda za Urusi na Iran kwa watu wa Syria na taifa lao." Inasomeka taarifa ya pamoja kutoka kwa Jeshi Huru la Waasi wa Syria na wanaharakati wa upinzani iliyotolewa leo.

Makundi hayo yanapinga mazungumzo hayo ya Cairo kwa kuwa yanakataa kuchukuliwa hatua za nguvu kuuondoa utawala wa Rais Assad kama suluhu ya kuokoa maisha ya raia wanaokufa kila siku. Pamoja na hayo, mkutano huo unatupilia mbali suala la vikwazo vya kijeshi dhidi ya Syria, na mpango wa kuwapa silaha waasi.

Mauaji yaendelea

Waasi na wanaharakati nchini Syria wameongeza kuwa mkutano huo wa Cairo una lengo la kuendelea kumshawishi Assad kuutii mpango wa amani wenye vipengele sita wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu unaosimamiwa na Kofi Annan, lakini washiriki wamesahau kuwa tangu kuanza kwa mkakati huo tayari maelfu ya watu wameshauawa.

Wanausalama wakizima moto magari yaliyoungua kwa bomu mjini Damascus.
Wanausalama wakizima moto magari yaliyoungua kwa bomu mjini Damascus.Picha: Reuters

Makubaliano ya kuwepo kipindi cha mpito nchini Syria hayakutoa wito malumu kwa Rais Assad kuachia madaraka kama yanavyopendekeza mataifa ya magharibi, baada ya Urusi na China kushikilia msimamo kuwa Wasyria wenyewe ndio wafanye maamuzi namna gani kipindi hicho kiwe.

Zaidi ya watu 79 wameuawa jana katika maeneo mbalimbali ya Syria kutokana na mashambulizi ya mizinga na risasi tangu jana.

Wanaharakati wanasema kuwa raia wengi wamezingirwa kwenye maeneo ya Joura al-Shia na Khalidiyya wakiwa hawana chakula na madawa.

Mwandishi: Stumai George/ AFPE/APE
Mhariri: Mohammed Khelef